SERIKALI YAENDELEA NA JITIHADA ZA KUBORESHA SEKTA YA SHERIA NCHINI- DKT BITEKO

MUUNGANO   MEDIA
0

 




Na Avelina Musa - Dodoma.


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko amesema Serikali inaendelea na jitihada za kuboresha sekta ya sheria nchini kwa kuajiri Maafisa Sheria, Mawakili wa Serikali pamoja na Mahakimu lengo likiwa ni kuhakikisha huduma bora inawafikia wananchi.


Dkt. Biteko amesema hayo leo Aprili 15, 2025 Jijini Dodoma katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali ambapo pia amewataka Mawakili wa Serikali kufanya kazi kwa kuzingatia taaluma na haki ili kusaidia Watanzania .

"Ombi langu kwenu Mawakili wa Serikali fanyeni kazi yenu kwa kuzingatia taaluma yenu ya sheria na haki, ni wajibu wenu kushauri kwa haki na fanyeni kazi bila kuogopa,fanyeni kazi ya kutetea Serikali yenu, nendeni mkaishauri Serikali"Amesema Dkt Biteko.



Dkt.Biteko amesema Serikali inatambua jitihada zinazofanywa na mawakili pamoja na Asasi  na binafsi katika kuwahudumia wananchi kupata huduma za kisheria.


Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni. Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Palamagamba Kabudi amewapongeza waasisi wa Chama hicho kwa kujenga taswira nzuri huku akiwaasa viongozi wengine watakao fuata kuendeleza taswira hiyo na amewataka mawakili hao kuwa marafiki wa Mungu badala ya Mahakama kwa kutenda haki na kusema kweli.


Mhe. Kabudi amesema  umuhimu wa mkutano huo wa Mawakili wa Serikali  ni kutoa fursa kwao ya kukutana na kujadiliana masuala ya kitaaluma, maslahi yao pamoja na kufahamiana.



Aidha,Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Hamza Johari amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kukilea chama hicho kwa miaka mitatu na kusema kuwa ni wajibu wao sasa kukilinda na kuhakikisha kinafikia malengo yake.



"Tumetengeneza Mpango Mkakati tunaokwenda kuutekeleza kwa shauku kubwa pamoja na viongozi wapya watakao chaguliwa katika Uchaguzi unaofanyika leo,” amesema Mhe. Johari.

Mhe, Johari amesema hadi kufikia Aprili 9, 2025 idadi ya Mawakili wa Serikali waliosajiliwa katika Daftari la Mawakili wa Serikali imefikia 3,760 kutoka 2,652 waliosajiliwa wakati wa kuanzishwa kwa Chama hicho.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Zanzibar, Mhe. Dkt. Mwinyi Talib Haji amewaomba Mawakili na Maafisa Sheria wa Serikali kufanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia sheria ili kujenga jamii imara na kupunguza mizozo katika jamii.



Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)