Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuongeza kasi ya uendelezaji wa Vitalu vya utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia ikiwemo Mnazi Bay Kaskazini, Eyasi Wembere, Songo Songo Magharibi na Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (LNG) ili nchi iendelee kuwa na uhakika wa upatikanaji wa nishati kwa ajili ya soko la ndani na nje.
Dkt.Biteko ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akizindua Mkakati wa Muda Mrefu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wa miaka 25 (2024/25 hadi 2049/50) ambao umeweka mipango na malengo makubwa ya kuleta uhakika wa upatikanaji wa nishati nchini, mkakati ambao utaisaidia nchi kutumia kikamilifu rasilimali za mafuta na gesi zilizopo katika maeneo mbalimbali.
”Tunapozindua Mpango Mkakati huu wa miaka 25, ni muhimu tutambue kuwa jukumu muhimu la TPDC ni kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa nishati nchini. Ni muhimu sisi sote hapa tukumbuke kuwa Sekta ndogo ya Mafuta na gesi ina mchango mkubwa sana katika maendeleo ya Taifa hili.” Amesema Dkt. Biteko
Aidha, Dkt. Biteko ameiagiza TPDC kuimarisha mtandao wa mabomba na mifumo ya usambazaji wa gesi nchini ikiwemo kupitia teknolojia za Mini-LNG na CNG ili kuwafikia wananchi wengi ambao wapo mbali na Bomba la Usafirishaji wa Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ili kusaidia kuwafikishia watanzania manufaa yatokanayo na matumizi ya gesi asilia.
Pia ameitaka kujiimarisha kifedha ili kuweza kutekeleza miradi mbalimbali kwa kubuni mifumo ya ubunifu ya utekelezaji wa miradi, kuboresha shughuli za kibiashara, na kuendelea kupunguza utegemezi kwa ufadhili wa Serikali ambapo ameipongeza kwa kuanza kujilipa mishahara kwa kutegemea fedha za Shirika.
Dkt.Biteko ameitaka TPDC kudumisha uwazi, uwajibikaji, na kuzingatia kanuni za mazingira, jamii, na utawala (ESG) na kufanya kazi kazi kwa karibu na kampuni za kimataifa za nishati, wawekezaji binafsi, na wadau wa maendeleo ili kuvutia mtaji, utaalamu, na teknolojia inayohitajika kwa mafanikio ya mpango uliozinduliwa.
Dkt. Biteko amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kuendeleza Sekta ya Nishati ambapo kupitia uongozi wake, ametekeleza miradi mingi ikiwemo kukamilisha Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) na kuhakikisha kunakuwa na uhakika wa upatikanaji wa nishati ya mafuta na gesi asilia hapa nchini na hivyo kuleta maendeleo endelevu ya Taifa na wananchi kwa ujumla.
Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, Dkt. Biteko ameiagiza TPDC kuhakikisha wanalipa kipaumbele suala la nishati hiyo kwa kuendelea kusambaza gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya kupikia na hivyo kupunguza hewa ukaa na uchafuzi wa mazingira kutokana na matumizi ya mkaa na kuni.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Nishati na Madini katika Serikali ya Mapiduzi Zanzibar, Shaib Kaduara ameeleza kuwa mkakati huo unatoa mwanga wa kukua kwa uchumi wa watanzania na kielelezo cha mafanikio yanayopigwa katika Sekta ya Nishati akisisitiza kuwa amani na umoja ndiyo msingi wa maendeleo.
Aidha, amempongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Dkt. Doto Biteko kwa maendeleo yanayofanyika na kuisimamia vyema Sekta ya Nishati.
Amesema kuwa kuzinduliwa kwa mpango huo kunatoa mwanga kwa miradi ya Gesi Asilia kufika maeneo mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Dodoma akieleza kwamba Mkoa upo tayari kupokea miradi ya gesi asilia kwa ajili matumizi mbalimbali ikiwemo kupikia na kuendesha vyombo vya moto ikiwemo magari.
Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Balozi Ombeni Sefue alisema kuwa Mpango Mkakati huo wa muda wa miaka 25 unakwenda sambamba na Ilani ya Chama cha Mapinduzi kuhusu masuala ya nishati, unalingana kwa karibu na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, hasa katika maeneo ya kuimarisha sekta ya nishati kama kichocheo kikuu cha uchumi wa viwanda, maendeleo ya miundombinu, kukuza matumizi ya teknolojia bunifu, kuongeza ajira na mapato ya Serikali, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, safi na nafuu kwa Watanzania wote.
“Kwetu sisi, hili siyo andiko tu kama maandiko mengine ya awali bali ni mwongozo madhubuti wa kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Nishati ya kufanikisha upatikanaji na usalama wa nishati na hivyo kuboresha maisha ya watanzania na kukuza uchumi endelevu.” Amesema Balozi Sefue.