CAG :AWASHAURI WATANZANIA KUSOMA RIPOTI YA UKAGUZI KWA MWAKA WA FEDHA 2023/24

MUUNGANO   MEDIA
0



Na Avelina Musa - Dodoma.


MKAGUZI na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali(CAG), Charles Kichere amewashauri watanzania kusoma Ripoti za ukaguzi wa hesabu za serikali kwa mwaka wa fedha 2023/24 kupitia jarida Maalum lililoandaliwa na Tovuti ya CAG kwa makini na kuona mambo yanayotekelezwa na Serikali yao.


CAG.Kichere ametoa Ushauri huo leo Aprili 16,2025 Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano wake wa uwasilishaji wa Ripoti za Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa Fedha 2023/24.


CAG Kichere amesema watanzania wasome Ripoti hiyo ili wajue jinsi serikali yao inavyotekeleza majukumu yake ambapo anasema tayari wameanza majadiliano na bunge ili kuona namna ya kuweka utaratibu wa kuanza kujadili ripoti hizo mapema zaidi kuliko hivi sasa ili ziweze kufanyiwa kazi zikiwa bado za moto.


“Mwanzo muda ulikuwa mrefu zaidi, ukapunguzwa na sasa tulishaanza majadiliano ipungue na ziwe zinajadiliwa mapema zaidi, nashauri ikimpendeza spika ripoti za mwaka huu zijadiliwe mapema zaidi kabla ya kuvunja bunge kuelekea uchaguzi mkuu,”amesisitiza Kichere.


Amesema tayari amewasilisha ripoti 14 za ufanisi katika sekta mbalimbali huku akiwataka wanahabari na wananchi kwa ujumla kusoma ripoti hizo na kuzielewa.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe,Oran Njeza amempongeza CAG kwa kuwa na timu nzuri ya wakaguzi ambayo inafanya kazi kwa ufanisi mkubwa, hadi kufikia Tanzania kufanya ukaguzi wa kimataifa.


Aidha, Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) Mhe.Halima Mdee amesema watumishi wanapaswa kuhakikisha wanazitatua dosari zinazobainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa kutoa taarifa sahihi zinazoendana na thamani ya fedha zilizotolewa na serikali katika kutekeleza miradi.


Mwisho.

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)