WMA YAFANIKIWA KUHAKIKI IDADI KUBWA YA MATENKI YA MAGARI.

MUUNGANO   MEDIA
0

 






Na Avelina Musa - Dodoma.

Katika kipindi cha awamu ya sita Wakala wa Vipimo (WMA)imefanikiwa kuhakiki idadi kubwa ya matenki ya magari yabebayo vimiminika shughuli ambayo inafanywa kupitia kituo kikubwa cha uhakiki wa vipimo cha Misugusugu. 

Kituo hicho ni moja ya vituo vya kisasa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ambacho kina uwezo wa kupima matenki ya malori 60 kwa siku.


Kauli hiyo imetolewa na Afisa Mtendaji Mkuu Wakala wa Vipimo (WMA)Bw.Alban Kihulla  leo Jijini Dodoma Machi,25,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka minne ya serikali ya awamu ya sita.

Kihulla amesema Wakala imefanikiwa kuhakiki vipimo 3,668,149 vitumikavyo katika sekta mbalimbali nchini kati ya vipimo 3,923,652 ilivyopanga kuhakiki ambayo ni sawa na asilimia 94 ya lengo. 

"Kati ya vipimo hivyo vilivyohakikiwa, vipimo 102,969 vilikutwa na mapungufu ambayo yalirekebishiwa kuendelea kutumika na vipimo 5,607 vilikataliwa kutumika baada ya kuonekana na mapungufu ambayo hayarekebishiki"Amesema Kihulla.

Amesema Wakala imejenga majengo mapya ya ofisi katika Mkoa wa Mara na Simiyu. Vile vile, ujenzi wa ofisi hizo umefanyika katika Mkoa wa Dodoma ambapo ujenzi wa jengo ambalo sasa linatumika kama ofisi za Wakala wa Vipimo Makao Makuu ulikamilika Machi, 2025 kwa shilingi billion 6.99.

"Wakala imeendelea kununua vifaa vya kitaalam kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma ikiwemo Iron Weight 500kg (100) kwa ajili ya kufanyia uhakiki na ukaguzi wa mizani kubwa zinazotumika viwandani na kwenye barabara na mitambo mikubwa miwili na mitambo midogo 10 inayobebeka kwa ajili ya uhakiki dira za maji"Amesema.

Aidha ameongeza kuwa Wakala wa Vipimo imenunua mitambo 12 kwa ajili ya kuhakiki vipima mwendo kwenye vyombo vya usafiri, kati ya mitambo hiyo, mitambo 10  inabebeka ambayo itasambazwa kwenye mikoa.


Mbali na hayo, kwa mwaka wa fedha 2024/25, Wakala inatarajia kuchangia kwenye mfuko Mkuu wa Serikali zaidi ya shilingi bilioni 7 ambapo kufikia Februari, 2025, Wakala imechangia kiasi cha shilingi bilioni 3.8. 

Mwisho.




Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)