Na Avelina Musa - Dodoma
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi Tanzania (UWT) Bi Mary Chatanda amelaani tukio la chambulio la Mwenezi BAWACHA wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bi Siglada Mligo lililotokea tarehe 25 machi,2025 Mkoani Njombe.
Bi Chatanda ametoa kauli hiyo mapema Leo machi 28 mwaka huu katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya tukio hilo lililosababisha maumivu yaliyopelekea kulazwa kwa mwanamke huyo.
Bi Chatanda amelitaka Jeshi la Polisi kuendelea kumsaka mtuhumiwa na kumfikisha katika vyombo vya sheria kwakuwa wapo tayari kutoa msaada wa kisheria kwa kutoa mwanasheria ili haki iweze kupatikana kwa mhanga wa tukio hilo.
"Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe kuendelea kumsaka mtuhumiwa na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria,UWT ipo tayari kumuwekea mwanasheria ili haki iweze kupatikana." Amesema Chatanda
Bi Chatanda amesema anashangazwa na ukimya wa viongozi wa Baraza la Umoja wa Wanawake wa Chadema juu ya shambulio la kudhuru mwili kwa kiongozi wa ngazi ya juu wa baraza hilo kwa nafasi ya mwenezi.
"Kutokemea matumizi ya nguvu kwenye tofauti ya kisiasa ndani ya chama hiko ni dalili ya uoga dhidi ya mfumo dume wa chama cha Chadema.
Aidha ameiomba ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa kufuatilia kwa karibu uanzishwaji wa madawati ya jinsia kwa vyama vya siasa na kuangalia utekelezaji wa majukumu yake ili madawati hayo yawe na uwezo na mamlaka ya kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya unyanyasaji na ukandamizaji dhidi ya wanawake kwakuwa sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2023 imevitaka vyama vya siasa kuanzisha madawati hayo.
Hata hivyo Bi chatanda amewahamasisha wanawake kujiandaa na kujitokeza muda ukifika wa kuchukua fomu za nafasi ya ubunge wa majimbo na udiwani
wa kata ndani ya vyama mbali mbali kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu 2025.