GST YAPANGA KUJENGA MAABARA YA KISASA DODOMA ILI KUCHOCHEA UKUAJI WA SEKTA YA MADINI.

MUUNGANO   MEDIA
0

 






Na Avelina Musa - Dodoma.

TAASISI ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imepanga 
kujenga maabara ya kisasa katika Mkoa wa Dodoma kwa ajili kuimarisha uchunguzi wa  sampuli za madini nchini ili kuchochea shughuli za utafiti na kuhamasisha ukuaji wa Sekta ya Madini. 

Maabara husika  itakuwa na vifaa vya kisasa na itaweza kufanya uchunguzi wa sampuli za madini nyingi zaidi ikiwemo zinazojumuisha madini muhimu na kimkakati.

Hayo yameelezwa leo March 27. 2025 na Kaimu Mtendaji Mkuu wa GST ,Bw.Notka Banteze Jijini Dodoma,wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Taasisi hiyo.

Banteze amesema, GST imefanikiwa kufanya utafiti wa madini ya helium  katika mikoa ya Arusha , Manyara, Dodoma, Singida na Shinyanga na kubaini kiwango cha helium katika chemchem za majimoto zinazofaa kwa hatua ya utafiti wa kina katika maeneo ya Ziwa Natron na Eyasi.

Akizungumzia kuhusu maendeleo ya tafiti za jiolojia , jiokemia na jiofizikia amesema mpaka kufikia mwaka 2024 , utafiti wa madini ya viwandani ulikamilika  ambapo jumla ya madini viwanda 44 yalibainishwa.

Kwa upande wa machapisho ya utafiti , Banteze amesema GST imefanikiwa kuchapisha vitabu viwili ambavyo ni kitabu cha madini yapatikanayo Tanzania toleo la tano  pamoja na kitabu cha madini viwanda toleo la pili pamoja ramani za maeneo husika.



Akielezea kuhusu mafunzo kwa wachimbaji wadogo, Banteze amesema GST imekamilisha utoaji wa mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini 2733 yaliyohusu uchukuaji wa sampuli wakilishi na utambuzi wa jiolojia ya maeneo yenye uwepo wa madini katika mikoa ya Lindi,Morogoro,Geita na Mwanza.

Banteze ameeleza, mwelekeo wa Serikali kupitia GST katika mwaka 2025/2026   GST imepanga kufanya utafiti wa kina kwa kutumia ndege ili kuongeza asilimia  za utafiti wa kina kutoka asilimia 16 mpaka 34 , ikiwa na lengo la kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.


Aidha, amesema  GST imepanga kujenga majengo ya kisasa ya maabara na ofisi katika mikoa ya Geita na Mbeya ili kuwasogezea huduma karibu zaidi wachimbaji madini ikiwemo wachimbaji wadogo wa madini. Kukamilika kwa ujenzi huo kutaongeza tija kwa wachimbaji wa madini kwa kuwapunguzia kuchimba kwa kubahatisha. 

Hata hivyo, Banteze amesema  GST imekusudia kukamilisha ujenzi wa mfumo wa usimamizi wa taarifa na takwimu za Taifa za madini. Kukamilika kwa mfumo huo utaongeza ufanisi katika utunzaji na usambazaji wa taarifa za madini na hivyo kuchochea uwekezaji katika sekta ya madini.



Mwisho.

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)