Na Avelina Musa - Dodoma.
Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imesema Tanzania itakuwa Nchi mwenyeji wa kongamano la Kimataifa la eLearning Afrika linalotarajiwa kufanyika Mei 07 hadi 09, 2025 katika kituo cha mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es salaam.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda leo machi 29,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma, ambapo amesema kongamano hilo linalenga kuwaleta pamoja wadau mbalimbali kutoka nchi 65 za Afrika.
Prof.Mkenda amesema Kongamano Hilo ni kwa ajili ya kujadili,kubadilishana uzoefu,kuhamasisha uwekezaji na kuazimia mipango ya pamoja ya kuchagiza matumizi ya Teknolojia za kidijitali katika sekta ya Elimu barani Afrika.
“kongamaono la 18 la eLearning afrika litafanyika katika kituo cha kimataifa cha Julius Nyerere jijini dar es salaam kuanzia mei 07 hadi 09 mwaka huu,tangu kuasisiwa kwake mwaka 2005 kongamano hili lishafanyika nchi 17 ikiwemo Tanzania.
“Kwa Tanzania kongamano hili lilifanyika mwaka 2021 hivyo mwaka huu litakuwa linafanyika kwa mara ya pili na linalenga kuwakutanisha wadau zaidi ya 1500 kutoka zaidi ya Nchi 65 barani Afrika”,amesema.
Aidha amesema makundi hayo ya wadau yatajumuisha watunga sera,watoa maamuzi,wataalamu wa Elimu,wataalamu wa Teknolojia,watafiti,wabunifu,wafanya biashara,wawekezaji na wadau wa maendeleo.
Prof.Mkenda amesema kongamano hilo litajumuisha mkutano wa mawaziri zaidi ya 50 kutoka nchi 49 barani Afrika utakao kuwa na lengo la kuazimia mikakati ya pamoja na kuandaa nguvu kazi mahiri katika kubuni, kuzalisha,na kuimalisha matumizi ya kidigitali.
“kama wenyeji wa kongamano hili nchi yetu inatarajia kunufaika na fursa mbalimbali kutokana na kuwa mwenyeji wa kongamano hili ambapo tutabaini mkakati mpya hususani katika sekta ya Elimu”,amesema.
Kongamano hilo litaenda sambamba na kaulimbiu isemayo “kufikiria upya Elimu,na maendeleo ya rasilimali watu kwa ustawi wa Afrika”