Na Avelina Musa - Dodoma.
SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC)limesema Uendeshaji wa Reli ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma umeendelea kwa ufanisi mkubwa na Shirika kupitia maelekezo mbalimbali ya viongozi limeendelea kuboresha utoaji wa huduma ya kusafirisha abiria.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania(TRC)Bw.Masanja Kadogosa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa shirika hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita Leo Machi 22.2025, Jijini Dodoma
Bw.Kadogosa amesema Malengo ya Shirika yaliyoanishwa kupitia Ibara ya 59 (d) na (e) ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 – 2025 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa 2021/22 – 2025/26 ni kutekeleza miradi ipatayo 15 ikwemo miradi ya ujenzi reli ya kisasa ya SGR.
Amesema wakati Serikali ya Awamu ya Sita inaingia madarakani, ujenzi wa mradi wa SGR ulikuwa ukitekelezwa katika vipande viwili (2) vya Dar es salaam hadi Morogoro ambapo utekelezaji wake ulikuwa umefikia 83.55% na Morogoro hadi Makatupora ulikuwa umefikia 57.57%.
"Mnamo Aprili 22, 2021, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliwaahidi Watanzania kuwa Serikali itakamilisha ujenzi wa reli ya SGR kutoka Dar es Salaam mpaka Makutopora na kuanza ujenzi wa vipande vingine"Amesema Kadogosa.
"Serikali ya Awamu ya Sita ilianzisha ujenzi wa reli ya kisasa kwa vipande vipya vitano; vipande vitatu (3) ni katika kukamilisha ujenzi wa reli ya SGR awamu ya kwanza kati ya Dar es salaam na Mwanza ambavyo ni Makutupora hadi Tabora (Km 368), Tabora hadi Isaka (Km 165), Isaka hadi Mwanza (Km 341)."Amesema.
Aidha Bw. Kadogosa amesema Jumla ya thamani ya mikataba iliyosainiwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya SGR ni takribani Dola za Marekani Bilioni 11.6 sawa na Trillioni 29.580.
Ujenzi wa reli ya SGR kwa awamu ya kwanza kati ya Dar es Salaam hadi Mwanza wenye jumla ya kilometa 1,596 umegawanyika katika vipande vitano (5).
"Kipande cha tatu, Makutupora – Tabora (Km 368), ujenzi umefikia asilimia 14.53, kipande cha nne, Tabora – Isaka (Km 165), ujenzi umefikia asilimia 6.61 na kipande cha tano, Isaka – Mwanza (Km 341) ujenzi umefikia asilimia 63.10."Amesema.
Bw.Kadogosa amesema Uendeshaji wa reli ya SGR kati ya Dar es salaam hadi Dodoma ulianza mnamo tarehe 14 Juni 2024 kati ya Dar es salaam na Morogoro na tarehe 25 Julai 2024 kati ya Dar es salaam na Dodoma. Hadi sasa, jumla ya abiria waliosafirishwa ni takribani milioni 2.1 na kiasi cha shilingi bilioni 59 zimekusanywa kama mapato.
"Sekta ya uchukuzi hususani kwa njia ya reli ni moja ya kichocheo cha kukuza uchumi na ni chanzo cha kuongeza mapato ya Taifa kwa njia moja au nyingine. Kwa namna ya pekee tunaishukuru na kuiomba Serikali iendelee kuwekeza katika uboreshaji wa miundombinu ya usafirishaji ili kuchagiza ukuaji wa uchumi wa nchi"Amesema.
Mwisho.