Na Avelina Musa - Dodoma.
Katika kipindi cha Miaka minne ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Benki ya Maendeleo (TIB) imefanikiwa kuwekeza zaidi ya Shilingi bilioni 630.3 katika miradi ya maendeleo hadi kufikia Desemba 2024.
Hayo yameelezwa Leo Machi 20, 2025 Jijini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo TIB, Bi.Lilian Mbassy, wakati akitoa taarifa ya mafanikio ya Taasisi hiyo na mwelekeo wake.
"Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia uwekezaji huo mkubwa zaidi ya ajira mpya 12,547
zimezalishwa kutokana na Benki kufadhili miradi ya muda wa kati na mrefu nchini"Amesema Bi.Lilian.
Bi. Lilian amesema uwekezaji huo umegusa maeneo ya kipaumbele ya Serikali pamoja na
Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) hasa katika Shilingi 162.7 bilioni zimewekezwa
kuongeza usalama wa chakula na kupunguza njaa, Shilingi 4.3 bilioni zimewekezwa
kuboresha elimu kupitia miradi ya taasisi za elimu, Shilingi 22.4 bilioni zimewekezwa
katika upatikanaji wa maji safi na usafi wa mazingira kupitia miradi ya mamlaka za maji.
“Katika mwaka 2025 Benki vipaumbele vyake vimejikita katika kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza sera na mikakati ya kitaifa ili kuongeza kasi ya maendeleo,
pamoja na kutekeleza vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita.
Aidha,Bi Lilian amesema Benki itaendelea kukuza mtaji wa Benki kwa kushirikiana na taasisi za
fedha za kimataifa ili kupata mikopo ya riba nafuu kwaajili ya kufadhili miradi mikubwa ya maendeleo yenye athari Chanya kwa jamii na uchumi.
Kupitia mradi wa upanuzi wa nishati ya umeme vijijini (Tanzania Rural Electrification
Expansion Programme-TREEP), Benki inaendelea kushirikiana na Benki ya Dunia kupitia REA, kutoa mikopo kwa wazalishaji wa nishati jadidifu wanaohudumia maeneo ya vijijini ambako umeme wa TANESCO haujafika.
Mwisho.