Na Avelina Musa - Dodoma.
Imeelezwa kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Mhe,Rais Dkt Samia Suluhu Hassan Serikali imewekeza shilingi bilioni 25.7 katika utafiti, ubunifu na maendeleo ya teknolojia kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 17/2025 Jijini Dodoma alipokuwa akielezea mafanikio ya tasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia suluhu Hassan.
Dkt.Nungu amesema Serikali kupitia taasisi hiyo imefadhili zaidi ya tafiti 50 katika sekta za Elimu, kilimo, afya, na mazingira ili kuhakikisha maarifa haya yanatumika kuboresha maisha ya Watanzania.
Amesema Serikali ya awamu sita imetoa fedha na kuweka mazingira rafiki kwa wanasayansi na wabunifu wa Kitanzania. Kupitia mfumo wa ushirikiano wa kimkakati kati ya serikali ya Tanzania na nchi rafiki pamoja na taasisi za kimataifa, COSTECH imepokea shilingi bilioni 5.65 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya utafiti wa pamoja kati ya watafiti wa Tanzania na washirika wetu.
''Hatua hii si tu kwamba imeendelea kuimarisha msingi wa maendeleo ya kisayansi, bali pia imethibitisha dhamira ya serikali ya kujenga taifa linalowekeza katika kuibua teknolojia, likiongozwa na tafiti na ubunifu'' amesema Dkt. Nungu.
''Kampuni mpya zipatazo 70 zimesajiliwa ikiwa na matokea ya wabunifu waliyowezeshwa na serikali yetu.'' amesema Dkt. Nungu.
Hata hivyo amesema katika historia ya Tanzania, serikali imetenga shilingi bilioni 6.3 kwa ajili ya miradi ya utafiti wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, huku shilingi milioni 600 zikielekezwa katika miradi minne ya usalama wa chakula.
Mwisho.