BMH YAELEZA MAFANIKIO LUKUKI KATIKA KIPINDI CHA MIAKA MINNE YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA.

MUUNGANO   MEDIA
0

 


Na Avelina Musa - Dodoma.


KATIKA kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imesema kumekuwa na Ongezeko la huduma za ubingwa wa juu kutoka 7 hadi 16 pamoja na huduma za kibingwa kutoka 14 hadi 20 ikiwa ni jitihada za kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya zenye ubora na gharama nafuu.


Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi leo Machi 04, 2025 Jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na utekelezaji wa majukumu ya hospitali hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.


Prof. Makubi amesema kuwa, BMH ikishirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) zimekuwa zikitoa na kupanua huduma za tiba za kibingwa na ubingwa wa juu wa tiba na upasuaji kwa wananchi wapatao milioni 14 kutoka mikoa zaidi ya 7 ya Tanzania ambapo katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Hospitali ya BMH ikitumia falsafa ya R4 imefanikiwa kuongeza huduma zaidi.


“Huduma za ubingwa zilizopo BMH kwa sasa zinajumuisha upandikizaji figo na matibabu yake, upandikizaji uloto, upasuaji wa mishipa ya damu, upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua, uvunjaji wa mawe kwenye mfumo wa mkojo kwa kutumia mawimbi na upandikizaji uume, upasuaji wa ubongo na mfumo wa fahamu, upasuaji wa uti wa mgongo, kubadilisha nyonga na magoti, upasuaji wa matundu madogo, matibabu ya mfumo wa chakula, uchujaji damu, matibabu ya magonjwa ya moyo, uchunguzi na matibabu ya mishipa ya moyo kupitia maabara ya uchunguzi, uchunguzi na matibabu ya kiradiolojia, tiba ya magonjwa ya homoni na kisukari pamoja na huduma za upandikizaji mimba”, amesema Prof. Makubi. 


Prof. Makubi amesema BMH imefanikiwa kuweka vipandikizi kwa wanaume watano ambao walikuwa na changamoto za upungufu wa nguvu za kiume, uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya mfumo wa chakula kwa wagonjwa 10,000, kuanzisha na kutoa tiba ya magonjwa ya homoni na kisukari kwa wananchi 11,404 pamoja na kutoa tiba kwa wagonjwa wa saratani kwa kutumia tiba kemia ambapo wananchi 12,000 wamehudumiwa.


Akielezea baadhi ya huduma hizo amesema, ndani ya miaka minne BMH imefanikiwa kupandikiza figo kwa wagonjwa 25, kupandikiza uloto kwa jumla ya watoto 20 waliokuwa na ugonjwa wa sikoseli, upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua kwa wagonjwa 60, upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu kwa wagonjwa 1061 ambapo kati yao, upasuaji wa ubongo 771 na upasuaji wa uti wa mgongo 290 na huduma ya kuvunja mawe kwa kutumia mashine maalumu ya mawimbi kwa wagonjwa 504.


Jumla ya wagonjwa 20,050 wamefanyiwa CT-Scan, 18,456 wamefanywa MRI, 99, 532 wamefanyiwa X-Ray na 134,622 wamefanyiwa Utrasound.


Aidha, huduma za tiba utalii zimetolewa kwa wagonjwa wa DRC, Comoro na Oman ambapo raia hawa wa kigeni hufika nchini Tanzania katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kupata matibabu ya kibingwa.


Hospitali hiyo kwa sasa ina jumla ya watumishi 967, kati yao madaktari bingwa 81, madaktari bingwa wa juu 16, madaktari wa kawaida 65 na wauguzi 412. 


BMH kwa siku inahudumia wagonjwa wa nje 1000 hadi 1200 na wastani wa wagonjwa 250 hadi 300 wanalazwa huku ikielezwa kuwa katika kipindi cha miaka minne, jumla ya wagonjwa 972,740 wamehudumiwa.


Mwisho

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)