WANAWAKE WAHIMIZWA KUGOMBEA

MUUNGANO   MEDIA
0

 


Na Avelina Musa - Dodoma.


KATIBU Mkuu wa Umoja wa wanawake Tanzania (UWT)Ndug,Suzan Kunambi(MNEC)amewataka wanawake wa Chama cha Mapinduzi kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2025.


Ndugu,Suzan amesema hayo jijini Dodoma leo Mei 24,2024 wakati akizungumza baada ya kupokelewa alipowasili katika Makao Makuu ya umoja huo ambapo katika mapokezi hayo viongozi mbalimbali wameshiriki wakiongozwa na Mwenyekiti wa umoja huo Mary Chatanda,Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Rosemary Senyamule pamoja na wabunge wanawake.


Amesema kuwa licha ya kuhamasishana wanawake kwenda kupiga kura lakini wanapaswa kujitokeza kugombea nafasi mbali mbali.


Aidha amesema kuwa maono ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ni makubwa sana katika maendeleo hivyo amewataka wanawake wa UWT kuyaelezea mazuri yanayofanywa na viongozi hadi yaeleweke ili yaache alama katika jamii.


“Naomba mnipe ushirikiano ili tuweze kutekeleza majukumu yetu na tuache alama zitakazoonekana vizazi na vizazi,”amesema Suzan.


Hata hivyo amewataka UWT kuhakikisha CCM inashinda maeneo yote katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu .


“Tunaanza na Serikali za mitaa tutahakikisha maeneo yote tunashinda ni lazima tukasake kura za CCM iwe jua iwe mvua na viatu au bila viatu lazima tushinde,”amesema Suzan.


Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Ndugu Merry Chatanda amesema UWT imejipanga kuhakikisha CCM inashinda kuanzia kwenye Uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu. 


Suzan aliteuliwa Mei 9,2024 baada ya Kamati kuketi chini ya Makamu Mwenyekiti wake ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi katika kikao chake maalum kilichofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar na kufanya uteuzi kwa niaba ya Halmashauri kuu ya chama hicho.


Mwisho.

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)