Wananchi
wa Kata ya Ngulugulu iliyopo wilayani Ileje wametakiwa kuendelea
kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za wahalifu na uhalifu
katika maeneo yao kwani huduma ya Polisi imeletwa karibu yao.
Kauli
hiyo imetolewa Mei 23, 2024 na Polisi Kata ya Ngulugulu Mkaguzi
Msaidizi wa Polisi Neema Minja wakati akizungumza na wananchi hao kwa
lengo la kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa ulinzi jirani katika maeneo
yao ili kuzuia uhalifu.
“Huduma ya Polisi kwa sasa inapatikana
katika ngazi ya chini kabisa kuanzia kata kwa hiyo ondoeni wasiwasi wa
kiusalama kuweni huru katika shughuli zenu za kila siku bila kuwa na
shaka kwani mimi nimeletwa kwa ajili yenu, mnachotakiwa ni kunipa
ushirikiano wa kutoa taarifa za uhalifu na vitendo vya ukatili wa
kijinsia ili kata yetu iendelee kuwa salama” alisema Mkaguzi Minja.
Aidha,
Mkaguzi Minja aliwasihi wananchi hao kuendelea kuimarisha ulinzi hasa
ukizingatia jiografia ya Kata hiyo inapakana na nchi jirani ya Malawi
hivyo kufanya kuwa na muingiliano wa wa watu ambao hawafuati utaratibu
wa kiserikali na kusababisha migogoro hasa ya ardhi pindi muwaonapo watu
hao toeni taarifa kwa viongozi ili waweze kushughulikiwa haraka ikiwemo
kufikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.