Na Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma.
Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya Dkt. Tumaini Haonga amesema Elimu ya Afya ya Uzazi kwa Vijana ina umuhimu mkubwa katika kuhakikisha kunakuwa na jamii salama.
Hivyo kutokana na umuhimu huo,ametoa wito kwa Watumishi wa Kituo cha simu cha Wizara ya Afya (Afya Call Centre-199), kuendelea kutoa ufafanuzi na elimu ya kutosha kwa vijana watakaopiga simu au watakaokutana nao wakiwa kwenye jamii , nyumbani, kwenye michezo, kanisani na maeneo mengine ikiwemo mitandao ya kijamii.
Dkt. Haonga amebainisha hayo Mei 24, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akifunga Mafunzo ya Afya ya Uzazi kwa Watumishi wa Kituo cha Simu cha Wizara ya Afya( Afya Call Centre )yaliyoanza Mei 20 na kuhitimishwa Mei 25.
Aidha, Dkt. Haonga amesema Mafunzo hayo yatasaidia kuongeza uelewa kuhusu utoaji wa elimu ya Afya ya Uzazi kwa Vijana Balehe.
“Nina imani kupitia kikao kazi hiki mtakuwa mmepata uelewa wa kutosha kuhusu masuala mbalimbali ya afya ya uzazi kwa vijana balehe na kwa kuwa ninyi mko kitengo cha elimu ya afya kwa umma, natarajia elimu mtakayoipata itafika maeneo mengine"amesema Dkt. Haonga.
Dkt.Haonga ameelezea matarajio baada ya mafunzo hayo kwa wananchi hususan vijana kuwa wataweza kupatiwa taarifa sahihi zaidi kuhusiana na masuala ya afya ya Uzazi.
Hali kadhalika, amelishukuru Shirika la Elimu, Sayansi, na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kwa kuwezesha mafunzo hayo kwa kushirikiana na wawezeshaji kutoka Wizara ya Afya, Idara ya Mama na Mtoto na kuomba ushirikiano huo uwe endelevu ili kuimarisha huduma za afya nchini.
Ikumbukwe kuwa Wizara ya Afya, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kwa kushirikiana na UNESCO imeratibu Mafunzo ya siku 5 ya Afya ya Uzazi kwa vijana kuanzia Mei 20-25, 2024 kwa watumishi wa kituo cha simu cha Wizara ya Afya (Afya Call Centre-199).
MWISHO.