Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) ametaja mafanikio ya Wizara katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania.
Mhe. Balozi Mbarouk ametaja mafanikio hayo jijini Dodoma Aprili 18, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari kuelezea mafanikio ya Wizara katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania.
Balozi Mbarouk amesema Wizara inajivunia kuendelea kuimarika kwa ushirikiano na uhusiano kati ya Tanzania na nchi mbalimbali duniani na hivyo kupata mafanikio katika sekta mbalimbali kupitia ushirikiano wa uwili na ujirani mwema baina yake na mataifa mengine.
“Mafanikio haya yamepatikana kupitia ushirikiano uliopo ambao unatekelezwa kupitia taratibu maalum ikiwemo mikutano ya Tume za Ushirikiano wa Pamoja. Ushirikiano huu umeleta mafanikio kupitia kusainiwa Mikataba na Hati za Makubaliano (MoUs) ili kutekeleza maeneo mahsusi katika sekta mbalimbali za siasa, kiuchumi na kijamii,”alisema.
Amesema Tanzania imefanikiwa kuwa sehemu ya kuanzishwa kwa jumuiya za kikanda kama Umoja wa Afrika; Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Nchi zilizo katika Maziwa Makuu (ICGLR) na kupitia uanachama katika jumuiya hizo Tanzania imetekeleza programu katika sekta mtangamano za siasa, ulinzi na Usalama; Miundombinu; Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji.
“Tanzania imekuwa sehemu ya utekelezaji wa dhana ya kutatua changamoto za kidunia kwa pamoja yaani Multilateralism, kuwa mbia anayeaminika na kukubalika katika maamuzi mbalimbali duniani hasa katika mashirika ya kimataifa hususan Umoja wa Mataifa na kuwa mbia kwenye vyombo mbalimbali ikiwemo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa; Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa; Benki ya Dunia na Shirika la Biashara Duniani (WTO),” alisema.
Ameongeza kuwa Tanzania imekuwa sehemu ya maamuzi katika maeneo ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi; ulinzi na usalama; utatuzi wa migogoro; maendeleo endelevu na utafutaji rasilimali kwa ajili ya maendeleo ambapo kupitia jukwaa hilo imepata fursa ya kutoa misimamo yake kwa masuala muhimu ikiwemo mgogoro wa Isarel na Palestina na suala la Sahara Magharibi na kuwa sehemu ya kuunga mkono Sera ya Kutofungamana na Upande wowote (NAM) na kuunga mkono ajenda ya msimamo wa Kundi la 77 na China katika majukwaa ya Kimataifa kwa maslahi mapana ya Taifa.
Amesema Tanzania inajivunia mchango wake katika juhudi za kulinda Amani Duniani na hivyo kutekeleza malengo ya Sera Mpya ya Mambo ya Nje na moja ya malengo mahsusi ya Umoja wa mataifa.
Amesema pia Tanzania imekuwa ikishiriki kulinda Amani kupitia Misheni za Kikanda ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC); Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa na baadhi ya maeneo ambayo Tanzania imechangia walinda amani ni pamoja na Lebanon; Darfur; Abyei; Liberia; Sudan Kusini; Sudan; DRC; Msumbiji na Afrika ya Kati na kuongeza kuwa Tanzania imeshiriki kikamilifu katika utatuzi wa migogoro kwa njia ya mazungumzo na diplomasia kwenye nchi na maeneo mbalimbali ikiwemo, Darfur; Cambodia; Sudan Kusini; Burundi na Kenya.
MWISHO.