Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt Dotto Biteko anatarijiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Mkutano wa 13 wa Kitaaluma wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) utakaofanyika Jijini Dodoma April 29 na 30 2024.
Hayo yamesemwa na Neville Meena Mjumbe kamati ya Utendaji Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) katika mkutano wake na Waandishi wa habari Jijini Dodoma wakati akielezea kufanyika kwa mkutano huo ambao utahudhuriwa na jumla ya Wahariri 150 kutoka vyombo mbalimbali vya Habari Nchini.
"Tutakuwa na mkutano wa kitaaluma wa 13,mikutano hii ya kitaaluma huwa inajadili mada Mahsusi kwa wakati huo. Sisi tumeanza miaka 14 iliyopita lakini kuna mwaka mmoja mkutano haukufanyika kutokama na mazingira kutoruhusu.
"Sasa mada kuu ama kaulimbiu inayoongoza mkutano wetu ni:''Nafasi ya vyombo vya habari katika matumizi ya Gesi,kwa ajili ya kulinda Misitu'' hii ndio kuu ambayo tumekuja nayo katika mkutano wetu wa kesho na kesho kutwa".Alisema Meena.
Aidha Meena amesema kuwa katika mkutano huo kutakuwa na mada mbalimbali za kitaaluma ambazo wanapaswa kuzijadili wao waandishi wa habari ikiwemo nafasi za wanawake katika vyumba vya habari lakini pia kuangazia masuala ya Uchaguzi ulioko mbele yetu kama vile uchaguzi wa Serikali za mitaa kwani waandishi wa habari ni wahusika wa masuala ya uchaguzi.
"Tutakuwa na mada zingine za kitaaluma zinazohitaji tuzijadili kama waandishi wa habari kama vile nafasi za wanawake katika vyumba vya habari,haki zao,wajibu wao pamoja na uzingatiaji wa Taaluma. Tutakuwa na Mada kuhusiana na Uchaguzi,kama mnavyofahamu mwaka huu kuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa,kwasababu tunahusika na masuala ya uchaguzi hivyo ni vema tukajiandaa kuhusiana na jambo hilo".
Aidha kwa upande wake Salim Saidy Salim mjumbe wa Kamati ya Utendaji Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha Waandishi wa habari kuwa wenye kuandika Habari za misitu na kufuatilia maendeleo yake na sio kutoa taarifa wakati wa kupandwa tu.
"Kwa mfano nawalaum sana Waandishi wa habari,ninyi vijana wangu mko hodari kuandika misitu wakati wa kupanda misitu kwa kusema kiongozi fulani kaongoza upandaji miche 1000 na mengineyo,lakini hatufanyi mwendelezo wa ufuatiliaji wa ile misitu tuliyopanda kwa kujua mungapi imeendelea kuwa hai,juhudi gani zinafanyika ili kulinda na kuelezea athari za kutokuwa na Misitu".
Huu ni mkutano wa 13 ambao utahudhuriwa na Wahariri 150 kutoka vyombo mbalimbali Nchini waliopo chini ya Jukwaa la wahariri TEF wenye Kauli mbiu inayosema:Nafasi ya Vyombo vya Habari katika Matumizi ya Gesi,Kwaajili ya Kulinda Misitu.
Mwisho.