Wanawake Wajasiriamali wenye mahitaji Maalum wakiwemo Wenye uoni hafifu, wasioweza kutembea kutoka Mikoa ya Pwani na Dodoma wanaoshiriki katika maonesho mbalimbali ya ujasiriamali kuelekea Siku ya Wanawake duniani katika Viwanja vya Mashujaa wameishukuru Wizara ya Afya, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kwa kuweka kipaumbele zaidi katika utoaji wa Elimu ya Afya pamoja na ugawaji wa vielelezo ikiwa ni pamoja na Vizibao (Reflectors) katika maonesho hayo.
Wakizungumza mara baada ya kupatiwa vizibao(Reflectors) hivyo, baadhi ya Wanawake Wajasiriamali hao wamesema vizibao hivyo vitasaidia katika kuepusha na ajali hasa kipindi giza linapoingia hasa wanapotoka kazini kwani waendedha wa vyombo vya usafiri ikiwemo magari na pikipiki watakuwa wanaona kiurahisi na kuweza kuchukua tahadhari .
“ Tunashukuru sana Wizara ya Afya kwa kutupa hivi vimeremeta vitatusaidia kututambulisha, tunapotaka kuvuka barabara watumiaji wengine wa barabara itakuwa rahisi sisi kutuona na kutuepusha na ajali na pia katika reflector hizi kuna ujumbe mahsusi namna ya kutambua afya zetu hasa afya ya Uzazi”anasimulia Regina Mbaji Mkazi wa Kibaha Mkoani Pwani.
Naye Hapiness Mataji mwenye ulemavu wa kuona kutoka mkoani Pwani anasema Wizara ya Afya imetoa mchango kwao .
“Nafurahi sana Wizara ya Afya imetupa kama kitambulisho tunapovuka barabarani wadereva wanatutambua haraka kwani ukivaa mavazi haya unaonekana haraka hata ukiwa mbali”amesema Hapiness.
Habiba Mohammed Issa yeye anasimulia kuwa pindi huduma za afya zitakapoanza kutolewa ikiwemo uchunguzi wa awali wa Saratani ya Mlango wa Kizazi zitakapoanza kutolewa katika mabanda ya Wizara ya Afya yupo tayari kwenda kupima afya huku akizungumzia namna vizibao vitakavyosaidia kuepusha ajali kwani ataonekana haraka na watumiaji wengine wa barabara pindi awapo barabarani.
Grace Msemwa ni Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya amesema upokeaji wa Vizibao umekuwa na mwitikio mkubwa huku akitoa wito kwa wananchi kupata fursa ya kutembelea mabanda ya Wizara ya Afya kuanzia Machi 7-11, 2024.
MWISHO.
.jpg)