Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango ametoa wito kwa washiriki wa Mkutano wa 21 wa Taasisi za Fedha
kutafakari kwa kina changamoto ya uhaba wa fedha za kigeni na hatua gani
za muda mfupi na wa kati zinazopaswa kuchukuliwa zaidi ya hatua za urekebu
zinazochukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 21 wa
Taasisi za Fedha unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha
(AICC). Amesema ni muhimu kwa Mkutano huo kujadili nafasi ya kutumia
viwango nyumbufu vya ubadilishanaji fedha (exchange rate flexibility) katika
kudhibiti uhaba huo wa fedha za kigeni.
Aidha Makamu wa Rais amewataka viongozi na wataalam katika sekta ya
fedha nchini kuhakikisha uwezo wa taasisi zao na sekta nzima unaimarika
zaidi ili kuhimili misukosuko inapotokea. Amewasihi kuangalia namna ya
kuimarisha zaidi Idara na vitengo vya utafiti na masoko ya kifedha nchini.
Amesema Menejimenti ya vihatarishi, usimamizi makini na ufuatiliaji wa
mwenendo wa benki moja moja na sekta nzima ni jambo la muhimu sana
katika kujenga sekta ya fedha iliyo imara na yenye uwezo wa kuhimili
misukosuko.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema Mkutano huo unapaswa kuangazia
njia za kudhibiti mikopo chechefu, kupunguza gharama za mikopo na kupanua
wigo wa mikopo nafuu hasa kwa wajasiriamali wadogo na wa kati katika sekta
za kilimo, mifugo, uvuvi, uchimbaji wa madini na viwanda vidogo. Pia
amesema sekta ya fedha inao wajibu wa kushiriki katika jitihada za kuhifadhi
mazingira na kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi kwani huathiri
uzalishaji na mapato hususan katika sekta ya kilimo, utalii, ufugaji na hata
uzalishaji katika viwanda vinavyotegemea malighafi zinazotokana na kilimo,
misitu na maliasili.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa taasisi zote za fedha kuimarisha jitihada za
kudhibiti madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na ukuaji wa kasi wa
teknolojia ikiwa ni pamoja na changamoto za utunzaji na usiri wa taarifa,
usalama wa mtandao wa kibenki, usambazaji wa taarifa potofu mitandaoni,
udhibiti wa fedha haramu pamoja na kuwalinda watumiaji kwa kushirikiana kwa
karibu na wadau wote.
Vilevile Makamu wa Rais amesema sekta ya fedha nchini kwa kiwango cha
kuridhisha imeweza kuhimili misukosuko ya kiuchumi iliyojitokeza katika miongo
miwili iliyopita na kupata mafanikio mazuri. Amesema takwimu rasmi za
maendeleo ya sekta ya fedha nchini na tathmini ya Shirika la Fedha la Kimataifa
(IMF) ya Disemba 2023 vinathibisha hivyo. Ametaja kwamba sekta kibenki iko
imara na ina mtaji na ukwasi wa kutosha huku inatengeneza faida. Ukuaji wa
mikopo iliyotolewa na mabenki kwa sekta binafsi umeongezeka kutoka 9.9%
mwaka 2021/22 hadi 22.2% mwaka 2022/23. Halikadhalika, uwiano wa mikopo
kwa sekta binafsi na Pato la Taifa ulifikia wastani wa 18.2% katika mwaka
2021/22 ikilinganishwa na 17.6% mwaka 2020.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Chande amesema
Serikali kupitia Wizara ya Fedha imeendelea kutekeleza jukumu muhimu
katika juhudi za kuimarisha sekta ya fedha kulingana na mpango mkuu wa
maendeleo ya sekta ya fedha wa mwaka 2020/2021-2029/2030. Pia amesema
Wizara ikiwa msimamizi mkuu wa sera za kiuchumi inashirikiana kwa karibu
na wadau wa sekta ya fedha kuendeleza hatua zinazokusudia kuimarisha
sekta ya fedha kwa kutunga na kutekeleza sera zinazoboresha mazingira ya
udhibiti, kuimarisha mfumo wa viashiria hatarishi na kukuza uwezo wa ndani
wa sekta ya fedha.
Aidha Chande ameongeza kwamba Sekta ya Fedha ya Tanzania imeonesha
uvumilivu katika kupambana na changamoto za uchumi wa dunia za hivi
karibuni. Amesema ufanisi huo unajionesha katika ukuaji wa rasilimali hasa
mikopo kwa sekta binafsi ambayo iliweza kukua kutokana na teknolojia za
kifedha za hali ya juu na hatua zilizochukuliwa na Serikali pamoja na Benki
Kuu za kuimarisha uchumi wa Taifa.
Akizungumzia uzinduzi wa Mfumo wa Taifa wa Malipo ya Papo kwa Hapo
(Tanzania Instant Payments System) Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania
Emmanuel Tutuba amesema uzinduzi wa mfumo huo unathibitisha dhamira ya
serikali ya awamu ya sita ya kutumia ipasavyo mifumo ya kielektroniki katika
kurahisisha mazingira mazuri ya biashara, kuongeza ufanisi katika utendaji
kazi na kupunguza gharama na muda katika kufanya malipo.
Ameongeza kwamba Katika kutekeleza adhma ya serikali, Benki Kuu ya
Tanzania imeendelea kusimamia mifumo ya malipo kwa wadau mbalimbali
pamoja na kudhibiti viatarishi mbalimbali vinavyoweza kujitokeza kupitia
mifumo ya malipo. Amesema Benki Kuu ya Tanzania imeweza kufanya ubunifu
wa kutengeneza mfumo huo wa TIPS ambao umezingatia viwango vya
kimataifa katika kutoa huduma kwa wananchi na kuwezesha ufanyaji miamala
ya kifedha kwa haraka na kwa gharama nafuu zaidi.
Mkutano huo wa unafanyika tarehe 07-08 Machi 2024 kwa kauli mbiu isemayo
“Kuimarisha Uwezo wa Sekta ya Fedha kuhimili misukosuko ya kiuchumi”.

