SERIKALI YATIMIZA AHADI YA KUPELEKEA UMEME WA UHAKIKA LINDI NA MTWARA
Ijumaa, Februari 09, 2024
0
Serikali imeendelea kutekeleza ahadi ya kupeleka umeme wa uhakika
katika mikoa ya Lindi na Mtwara ambapo leo Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba ameongoza mapokezi ya mtambo wa
megawati 20 utakaozalisha umeme kwa kutumia Gesi Asilia.
Mtambo huo aina ya TM16 wenye mfano wa injini ya ndege ya Boeing 747
utafungwa katika Kijiji cha Hiari, Wilaya ya Mtwara Vijijini ikiwa ni
maelekezo ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Wizara ya Nishati
kuhakikisha kuwa changamoto ya upatikanaji umeme kwenye mikoa hiyo
inatatuliwa.
Akipokea mtambo huo kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba,
amesema kuwa mtambo huo utaondoa changamoto ya upatikanaji wa umeme
kwenye Mkoa wa Lindi na Mtwara.
“ Mhe. Rais alitoa maelekezo kwa Wizara ya Nishati, kufanya kila
jitihada ili changamoto ya umeme kwenye mikoa hiyo itatuliwe kwa
haraka, tunashukuru leo tumeweza kutimiza ahadi hiyo kwani mtambo
huu ni miongoni mwa mitambo ya kisasa kabisa ya umeme iliyowahi
kuletwa nchini ambayo inatoa uhakika wa kuzalisha umeme kwa kipindi
kirefu.” Amesema Mha.Mramba
Aidha, Mhandisi Mramba ameongeza kuwa, maelekezo Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati kuhusu kuepeleka umeme wa gridi kwenye mikoa hiyo
yameshaanza kutekelezwa ambapo kabla ya mwezi wa sita mwakani umeme wa
Gridi ya Taifa utakuwa umefika kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara.
Kuhusu maelekezo aliyoyatoa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ya
kuhakikisha wananchi wa mikoa hiyo inayozalisha gesi kwa wingi
wananufaika na uwepo wa nishati hiyo, amesema tayari wameanza
kuboreshewa huduma mbalimbali ikiwemo kuwajengea kituo cha Polisi,
ununuzi wa boti ya kisasa kwa ajili ya usafiri wa wananchi eneo la
Songosongo mkoani Lindi na ujenzi wa kituo cha afya eneo la Madimba
mkoani Mtwara..
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas Ahmed alisema kuwa,
wananchi wa Mtwara wamepokea kwa furaha mtambo huo ambao utafungua
fursa za uwekezaji kwa kutokana na kuwepo kwa umeme wa uhakika kwani
takriban asilimia 80 ya matumizi ya umeme mkoani humo yanatumika
kwenye sekta ya biashara.
“ Tunamshukuru sana Mhe. Rais, Dkt. Samia kwa kutimiza ahadi yake na
na mapenzi ya dhati aliyoyaonyesha kwa wananchi wa mikoa ya Lindi na
Mtwara na kufanya mikoa hii kupata umeme wa uhakika ambao utainua
sekta ya uchumi kwa ujumla.” Amesema Kanali Ahmed
kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Nishati na Madini, Mhe. Kilumbe Ng’enda ameishukuru Serikali kupitia
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt Doto Biteko kwa
kusikiliza kilio cha wabunge wa mikoa juu ya changamoto ya upatikanaji
wa umeme wa uhakika na kuipongeza Wizara ya Nishati kwa hatua kubwa
inazochukua kuhakikisha sekta ya umeme inaimarika.
.jpg)
.jpg)