Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ametoa tamko hilo leo Februari 05, 2024
alipofanya ufuatiliaji wa Taasisi ya Ally-Habshi inayojishughulisha kutoa mafundisho ya Madrasa kufuatia
kukamatwa kwa Mwalimu wake Bw. Yusuph Mohamed kwa tuhuma za kukutwa akitoa mafundisho ya
Dini kwa watoto 132 kwenye mazingira hatarishi yasiyo na huduma muhimu za Kijamii.
Akizungumza na waandishi wa Habari wakati alipotembelea kituo cha kulelea watoto wenye uhitaji
kilichopo Kata ya Kikombo Jijini Dodoma ambacho ndicho watoto hao walipelekwa baada ya kutolewa
kwenye maeneo waliyokutwa Mtaa wa Sogeambele na Nkuhungu kufuatia kukamatwa kwa Mwalimu
wao.
Mhe. Senyamule amesema Serikali inatambua umuhimu wa Dini,Taasisi za Dini na nafasi ya viongozi wa
Dini zote katika kujenga kizazi chenye hofu ya Mungu na kuwa na maadili mema.
Hata hivyo, ameongeza kuwa Mafunzo ya Dini kwa watoto ni jambo lenye umuhimu mkubwa na
linaugwa mkono na Serikali kwani Mkoa unashirikiana kwa Karibu na viongozi wa dini katika mikakati
mbali mbali ya maendeleo ya Mkoa.
“Taasisi ni lazima kabla ya kuanzishwa, ifuate vigezo vyote vinavyotakiwa vya kijamii, naelekeza usajili na
uendeshaji wa makao ya watoto ufuate utaratibu.
“Taarifa ya awali ya ukaguzi wa miundombunu ya Taasisi hii imebainisha ukiukwaji wa sheria. Viongozi
wa mitaa na vijiji hakikisheni munatambua wageni wote wanaoingia katika maeneo ya utawala pamoja
na kufuatilia shughuli wanazozifanya” Amesema Mhe. Senyamule.
Tukio hilo lilitokea Februari Pili 2024 wakati Timu ya Mkoa ilipofika katika vituo vya Taasisi hiyo vilivyopo
maeneo ya Nkuhungu na Chihanga baada ya kupata taarifa ya uwepo wa vituo hivyo na kubaini baadhi
ya watoto ambao wametoka Dodoma na mikoa ya jirani kama vile Arusha na Manyara kupatiwa
mafunzo hayo.

