SERIKALI INAKAMILISHA MKAKATI WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA - MHE. KAPINGA

MUUNGANO   MEDIA
0


 Naibu Waziri wa  Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema kuwa, kwa sasa

Serikali inakamilisha kazi ya uandaaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi
ya Nishati Safi ya Kupikia kwa lengo la kuhakikisha kuwa asilimia 80
ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo Mwaka 2033.



Amesema hayo leo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe.
Jacqueline Ngonyani Msongozi (Viti Maalum) aliyetaka kufahamu mpango
wa Serikali wa kuweka ruzuku kwenye Nishati ya Gesi ili Wananchi
waweze kumudu kununua.

Akijibu swali hilo, Mhe. Kapinga amesema “Serikali inaendelea kuchukua
hatua mbalimbali kutatua vikwazo vinavyokwamisha matumizi ya nishati
safi ya kupikia ili kupunguza gharama za upatikanaji wa nishati safi,
vifaa na majiko sanifu ya kupikia.”

 Ameeleza kuwa, Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia ni Ajenda ya Rais,
Dkt. Samia Suluhu Hassan na hilo lilitiliwa mkazo katika Mkutano wa 28
wa Nchi Wanachama  wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP
28) Dubai, ambapo  Rais, Dkt. Samia alizindua mkakati wa nishati safi
ya kupikia kwa Wanawake Afrika hivyo Wizara ya Nishati inalibeba suala
la nishati safi ya kupikia kwa uzito mkubwa.

Kuhusu ruzuku kwa mitungi ya gesi ili kupunguza gharama ya mitungi
hiyo, Naibu Waziri amesema kuwa, tayari kuna programu na miradi
mbalimbali inayoendelea akitolea mfano programu ya ushirikiano na
Umoja wa Ulaya (EU) ambapo Mawakala wanawezeshwa kifedha ili kupunguza
bei ya mitungi ya gesi kwa watu wanaonunua mitungi hiyo kwa mara ya
kwanza na kwamba Serikali itaendelea kubuni miradi na kutafuta fedha
ili wananchi wapate gesi kwa gharama nafuu.

 Ameongeza kuwa, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa
ikibuni na kutekeleza Sera na Mikakati yenye lengo za kuhamasisha
matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na utunzaji wa mazingira.

 Vilevile, Mhe. Kapinga amesema kuwa, Serikali kupitia Wakala wa
Nishati Vijijini (REA) imeanza mradi wa kusambaza nishati safi ya
kupikia kwenye taasisi mbalimbali ikiwemo magereza, kambi za jeshi,
shule za msingi na Sekondari na kwamba zoezi hili ni endelevu kwani
Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuzifikia taasisi nyingi zaidi.



Mhe. Kapinga amesema kuwa, jitihada hizo zinazofanywa na Serikali ni
utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Nishati ya Mwaka 2015 inayoielekeza
Serikali kuchukua hatua madhubuti za kufanikisha matumizi ya nishati
na vifaa sahihi vya kupikia.

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)