Mhe. Askofu Dkt. Alex Malasusa, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania;
Mhe. Askofu Dkt. Fredrick Shoo, Mkuu wa KKKT Mstaafu na Askofu wa
Dayosisi ya Kaskazini;
Mhe. Askofu Dkt. Abel Godson Mollel, KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati;
Mhe. Askofu Mstaafu Dkt. Solomon Massangwa, KKKT Dayosisi ya Kaskazini
Kati;
Wahe. Maaskofu wote wa KKKT mliopo;
Wahe. Maaskofu na Viongozi wa Madhehebu mengine ya Kikristo;
Sheikh Shaban Juma, Sheikh wa Mkoa wa Arusha;
Mhandisi Robert Kitundu, Katibu Mkuu KKKT;
Mch. Canon Dkt. Moses Matonya, Katibu Mkuu Jumuiya ya Kikristo Tanzania;
Mch. Lareiton Lukumay – Msaidizi wa Askofu KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati
na Wasaidizi wote wa Maaskofu;
Makatibu wa Dayosisi za KKKT;
Wageni wote wa KKKT kutoka nje ya nchi;
Wachungaji na Wainjilisti;
Wenza wa Maaskofu;
Waheshimiwa Mawaziri mliopo;
Mhe. John Mongela, Mkuu wa Mkoa wa Arusha;
Mhe. Queen Sendiga, Mkuu wa Mkoa wa Manyara;
Wahe. Wakuu wa Wilaya wote mliopo;
Mhe. Mrisho Gambo, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini na Wahe. Wabunge
wengine mliopo;
Viongozi wengine wote wa Serikali mliopo hapa;
Wapendwa waumini wa KKKT;
Waandishi wa habari, Mabibi na mabwana
Bwana Yesu asifiwe...
Utangulizi
Mhe. Mkuu wa Kanisa, Maaskofu, Wachungaji na Waamini wote wa KKKT;
1. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha
kujumuika katika ibada hii maalum. Pili, nalishukuru Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania kwa kukubali nimwakilishe Mhe. Rais na Serikali katika ibada hii
maalum. Nafahamu kwamba Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ndiye mliyemwalika kuwa Mgeni rasmi katika ibada
hii. Lakini kutokana na kuzongwa na majukumu mengi ya kitaifa, amenituma
kumwakilisha.
2. Pamoja na tukio la leo, mwezi Januari, 2024 ilifanyika ibada maalum ya
kumuingiza kazini Mhe. Askofu Dkt. Malasusa kuwa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania. Napenda kutumia fursa hii kukupongeza sana Mhe. Askofu
Dkt. Malasusa kwa kuitwa na kukubali kutumikia tena katika nafasi ya Mkuu wa
3
KKKT. Tunakuombea kwa Mungu ili akuongoze katika kutekeleza majukumu
hayo mazito; maana yeye hatakuacha kama alivyoahidi katika Kitabu cha Nabii
Isaya, “Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana
mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika
kwa mkono wa kuume wa haki yangu.” (Isaya 41:10)
3. Napenda pia kutumia nafasi hii kumpongeza sana Mhe. Askofu Dkt. Shoo
ambaye alikuwa Mkuu wa KKKT kwa kipindi cha miaka 8 iliyopita. Serikali
inakupongeza Mhe. Askofu Shoo kwa kuliongoza Kanisa vema na kuendeleza
mahusiano mema na Serikali hadi ulipomaliza kipindi chako cha Mkuu wa
Kanisa. Serikali inakutakia heri katika Nimetaarifiwa kuwa ingawa umekabidhi
majukumu ya ukuu wa Kanisa, bado unaendelea kuwa Askofu na kiongozi wa
Dayosisi ya Kaskazini. Hivyo, Baba Askofu Dkt. Shoo nakupongeza sana na
ninakutakia baraka na heri katika kuendelea kumtumikia Mungu kwa uaminifu
katika nafasi yako ya Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini.
4. Kwa namna ya pekee, ninaleta kwa Mhe. Askofu Dkt. Abel Godson Mollel na
Msaidizi wako Mch. Lareiton, pongezi za dhati kutoka kwa Mhe. Samia Suluhu
Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchaguliwa kuongoza
Dayosisi hii ya Kaskazini Kati. Hatuna mashaka kuwa mtatekeleza kwa haki na
uchaji wa Mungu majukumu mliyokabidhiwa leo. Mungu mwenyewe
atawawezesha na kuwaongoza. Kama tunavyosoma katika kitabu cha Yeremia
33.3 aliahidi kwamba “Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonesha mambo
makubwa, magumu usiyoyajua”.
5. Aidha, ninatoa pongezi nyingi kwa Mhe. Askofu Dkt. Massangwa –aliyekabidhi
uongozi wa Dayosisi hii ya Kaskazini kati. Nimepewa taarifa kwamba yeye
alipokea Dayosisi katika mazingira tofauti kwani hakupata nafasi ya kukabidhiwa
na mtangulizi wake, Mhe. Hayati Askofu Dkt. Thomas Laizer. Pamoja na
mazingira hayo, kwa msaada wa Mungu alisimama imara na kwa kipindi cha
miaka kumi aliendeleza kwa umahiri kazi ya uinjilishaji. Hongera sana Mhe.
Askofu Massangwa, bila shaka Mungu unayemtumikia atakulipa kwa utumishi
wako kama ilivyoandikwa katika 1 Petro 5:4 kwamba “Na Mchungaji Mkuu
atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka”. Zaidi ya hayo,
nakutakia maisha mema ya uzee, ukafurahi na wajukuu huku ukiendelea kutoa
ushauri kwa Mhe. Askofu Mollel watumishi wengine.
6. Naomba kutumia nafasi hii kuwakumbusha Waamini wa Dayosisi hii na Wakristo
wote kuhusu wajibu wetu kwa Viongozi wetu wa kiroho. Waraka wa Timotheo
unatukumbusha kuwa: “Viongozi wa Kanisa wanaowaongoza watu vizuri
wanastahili kupata heshima mara dufu, hasa wale wanaofanya bidii katika
kuhubiri na kufundisha” (1 Tim 5:17). Aidha, Mtume Paulo anatuasa kuwa:
“Watiini viongozi wenu na kushika amri zao. Wao huchunga roho zenu usiku na
mchana, watatoa ripoti ya utumishi wao mbele ya Mungu. Kama mkiwatii
watafanya kazi kwa furaha, la sivyo watazifanya kwa huzuni na hiyo haitakuwa
na faida kwenu” (Waebrania 13:17). Nawaomba sana waamini wenzangu
4
kumpa Mhe. Askofu Dkt. Abel ushirikiano wa dhati ikiwa ni pamoja na
kumpenda, kumtii, kumtia moyo na kumwombea kwa Mwenyezi Mungu. Hivyo
hivyo, naiomba familia ya Mhe. Askofu Mpya, hususan Mke wake kumtunza,
kumpenda, kumsaidia na kuzidi kumwombea ili aweze kutenda kazi yake pasipo
vikwazo vya aina yoyote nyumbani.
Mhe. Mkuu wa Kanisa, Maaskofu, Wachungaji na Waamini wote wa KKKT;
7. Napenda kutumia hadhara hii kuwahakikishia kuwa, Serikali inayoongozwa na
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, itahakikisha kuwa wakati wote itasimamia na
kulinda haki ya kuabudu kwa wananchi wote bila ubaguzi. Aidha, itahakikisha
kwamba wananchi wanaendelea kuishi kwa amani na kupata huduma bora za
kijamii. Serikali itaendelea kuwekeza katika miradi mikubwa ya kimkakati katika
sekta zote, ambayo ikikamililika itachangia kwa kiasi kikubwa kuinua uchumi wa
Taifa letu. Nawaomba viongozi wa KKKT na madhehebu mengine kuendelea
kuiunga mkono Serikali ili kwa pamoja tuweze kumhudumia Mtanzania kimwili
na kiroho kama iwapasavyo watoto wa Mungu.
8. Kama mnavyofahamu, mwaka huu utafanyika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Uchaguzi huu ni muhimu kwa kuwa utatupatia viongozi katika mashina
wanakoishi wananchi kwa ajili ya kuchochea maendeleo na ustawi wa jamii.
Nawaomba viongozi wote wa dini nchini kusaidia kutoa hamasa kwa wananchi ili
wajitokeze kwa wingi kushiriki katika uchaguzi huo. Serikali inaahidi kufanya
jitihada za kuweka mazingira ya haki na wezeshi ili wananchi waweze kushiriki
kuchagua viongozi wanaowataka kwa amani na utulivu.
Mhe. Mkuu wa Kanisa, Maaskofu, Wachungaji na Waamini wote wa KKKT;
9. Serikali inajivunia ushirikiano mzuri uliopo kati yake na taasisi za dini ambao
umedumu kwa muda mrefu katika nyanja mbalimbali na inatambua na
kuthamini mchango mkubwa wa Kanisa katika utoaji wa huduma za jamii,
hususan elimu, afya na maji. Nimesikia ombi lako Mhe. Mkuu wa Kanisa juu ya
kuhuisha ushirikiano baina Serikali na la KKKT na madhehebu mengine katika
utoaji wa huduma katika hospitali ya Urkesumet na hospitali ya Selian (ALMC).
Napenda kukuahidi kwamba Serikali kupitia Wizara ya Afya itashirikiana kwa
karibu na KKKT katika kutatua changamoto zilizopo hivi sasa. Hivyo, naiagiza
Wizara ya Afya na TAMISEMI kukaa pamoja na viongozi husika katika Kanisa ili
kutafuta muafaka wa jambo hili na kuwasilisha ushauri Serikalini ili kulipatia
ufumbuzi suala hili.
Mhe. Mkuu wa Kanisa, Maaskofu, Wachungaji na Waamini wote wa KKKT;
10. Yapo mambo machache ambayo napenda kuwaomba kwa niaba ya Serikali,
myawekee msisitizo zaidi katika mafundisho na maonyo yenu ya Kimungu.
Jambo la kwanza, ni kulinda na kudumisha Amani, Umoja na Uhuru wa nchi
yetu. Tunu hizi za Taifa ndizo zinazotutambulisha sisi kama Watanzania popote
duniani. Kwa namna ya kipekee kabisa napenda kuwashukuru kwa kuendelea
kudumisha amani, umoja na uhuru wa Taifa letu. Pili, ni usafi na utunzaji wa
5
mazingira. Nawaomba Viongozi wa dini kuendelea kupaza sauti kuhamasisha
ulinzi na uhifadhi wa mazingira katika nchi yetu. Tukemee ukataji na uchomaji
hovyo wa misitu na uchafuzi wa mazingira katika maeneo mbalimbali.
Tuwahimize waamini na wananchi wote kuheshimu na kuzingatia matumizi bora
ya ardhi hususan maeneo ya kilimo, mifugo na vyanzo vya maji, na Nne,
tunatambua kuwa maendeleo hayawezi kuja bila kuwepo kwa ushirikiano.
Hivyo, nawahimiza kudumisha ushirikiano kati ya madhehebu mbalimbali ya dini
na Serikali pia.
11. Nimalizie kwa kuwapongeza tena Mhe. Askofu Dkt. Abel Mollel na Mch. Lareiton
kwa kupokea majukumu mliyopewa ya kumtumikia Mungu, na Kanisa katika
Dayosisi hii. Nawaomba wakristo wenzangu na wananchi wote tuwaombee
viongozi wetu hawa ili wadumu daima katika kumtumikia Mungu na awaepushe
na vikwazo mbalimbali.
Nawashukuru sana kwa ahadi yenu ya kuendelea kumuombea Mhe. Rais na sisi
wasaidizi wake ili tutimize vema majukumu yetu ya kuwatumikia Watanzania
kwa unyenyekevu na uchaji wa Mungu pia. Aidha, nitafikisha salamu zenu kwa
Mhe. Rais kama mlivyozitoa.
Asanteni kwa kunisikiliza.

