Baadhi ya Wakuu wa idara wilaya ya Mlele wakiwa kwenye kikao cha tathmini na maandalizi ya bajeti mpya ya mwaka wa fedha 2024/2025.Picha na Mary Clemence
Katavi.Serikali mkoani Katavi haitapokea au kuwasilisha wizara ya Tamisemi bajeti mpya ya halmashauri yeyote, isiyolenga kutatua kero za wananchi kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Hayo ni kwa mujibu wa Mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko leo Jumatano Februari 14,2024 akitoa mwelekeo wa serikali katika kikao cha tathmini na maandalizi ya bajeti mpya.
Utaratibu huo umeanzishwa ili kupata mwarobaini wa kero za wananchi zinazoibuka kwenye mikutano ya hadhara mbele ya viongozi wa kitaifa.
“Kabla bajeti hii hatujasonga nayo mbele kutoka kwenye ngazi ya mkoa kwenda taifa, Wakurugenzi na timu zenu hakikisheni zinajibu matatizo na sivinginevyo,”amesema Mrindoko akaongeza.
“Kila halmashauri ina kero zake kutokana na mazingira, idadi ya watu, miundombinu iliyopo,itathmini upya bajeti yake hususani inayotokana na mapato ya ndani,”
Awali Afisa kilimo halmashauri ya Mlele Luke Kifyas miongoni mwa wajumbe ametaja sababu inayochangia kutofikia lengo la ukusanyaji mapato ya ndani ni matamko ya kisiasa.
“Tuna ushuru wa karanga ghafi,kichele zilizomenywa,mpunga na mchele,mwaka jana tungefanya vizuri ukusanyaji mapato lakini wanasiasa walisema wananchi watatuonaje?,”
“Tulisitisha hizo tozo athari imekuja kwetu tumeshindwa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa baadhi ya maeneo, tutilie mkazo suala hili,”amesema Kifyasi.
Kauli hiyo ikawaibua Diwani wa kata ya Ilunde ambaye pia ni Mjumbe wa kamati ya fedha Martin Mgoloka na Soud Mbogo Mwenyekiti wa halmashauri ya Mlele wakikiri kuwepo hali hiyo.
“Tuliathirika,tumejadiliana kupitia kamati ya fedha tumeomba kuandaliwa kikao na wadau, ushirikishwaji wananchi mdogo, kelele zilikuwa nyingi wadau wa biashara hawakushirikishwa,”amesema Mgoloka.
“Tumeona hilo ndiyo maana rasimu ya Mlele tumetoka asilimia ishirini ya kwenda kwenye miradi ya maendeleo hadi kufikia arobaini, itakasaidia kutatua kero za wananchi tunaowasimamia,”amesema Mbogo.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Takukuru wilaya ya Mlele Leonida Mushema akaibua hoja ya kukosa ushirikiano wa kuonyesha madeni halisi yaliyopo kwenye mfumo.
“Naomba wataalam toeni vielelezo mlivyonavyo ili mlipwe hizo fedha, changamoto tunayokumbana nayo na inatuchelewesha wanaopewa kazi ya kukusanya mapato hawana mikataba,”
“Pia anapokabidhia posi hakuna kitabu kingine anachosaini wakati mwongozo unasema iandikwe, inatuathiri tunapoenda kwenye vyombo vya sheria wanaturudisha,”amesema Leonida.
Anna John mkazi wa mkoa wa Katavi amesema kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 kiu ya Wanakatavi kuona serikali inakamilisha miradi ya maendeleo.
“Wananchi wanasubiri huduma kuna ongezeko la watu ikilinganishwa na awali, bado shule hazitoshi na mengineyo matokeo ya sensa ni kipimo halisi cha mahitaji yaliyopo,” amesema Anna.
Kikao hicho kilichohudhuriwa na Wakuu wa idara na wilaya kutoka halmashauri zote, kimeazimia kila mtumishi kufanya kazi kwa mujibu wa sheria ili kutimiza adhima ya serikali.

