UTEKELEZAJI WA MIRADI YA ELIMU IENDANE NA MAZINGIRA SALAMA KWA WANAFUNZI.

MUUNGANO   MEDIA
0

 


Asila Twaha, Kigoma DC.

Wataalam kutoka Benki ya  Dunia  wamewashauri wasimamizi wa elimu nchini  kuzingatia  usalama wa watoto ndani na nje ya shule kwa  kuimarisha usimamizi wa  mazingira katika  maeneo ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi inayoendelea.


Hayo yamebainishwa na Mtaalam anayeshughulikia Masuala ya Jamii na Usalama kutoka Benki ya Dunia Dkt.Naima Besta kwenye  ziara ya kikazi  iliyowashirikisha  timu ya Wataalam OR- TAMISEMI, Wizara ya Elimu , Sayansi na Teknolojia na Wadau wa Benki ya Dunia lengo likiwa ni kukagua utekelezaji wa  miradi ya elimu SEQUIP na BOOST  Mkoani Kigoma.


Amewaelekeza wasimamizi wa elimu nchini kuzingatia usalama wa watoto na mazingira kwa kuwapa nafasi ya kujadili  changamoto zao kwenye mabaraza ya wanafunzi, kuwepo na walimu wa nasihi ambao watasikiliza na kushughulikia maoni yao.


"Usalama wa mtoto ni pamoja na shule hizo kuweka vibao vya matangazo ili kuonesha  ujumbe kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla" amesisitiza

Naye, Mratibu wa Shule Salama Ofisi ya Rais -  TAMISEMI Bi. Hilda Mgomapayo amesema, Serikali inaendelea kuboresha miundombinu kwa kuweka mazingira salama  kwa watoto  kuanzia Elimu  ya Awali,  Msingi hadi Sekondari kwa lengo la kuwezesha wanafunzi kukamilisha mzunguko wao wa elimu.


 Amesema mazingira salama ya mtoto ni pamoja na kuimarisha mfumo wa kushughulikia malalamiko ya wanafunzi, kuimarisha, mahusiano na ushirikiano kati ya shule na jamii katika kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, kudhibiti hali ya utoro  na kuimarisha huduma ya chakula shuleni. 


"Tuendelee kutoa elimu kuhusu usawa wa kijinsia,mapambano dhidi ya vitendo vya unyanyasaji na ukatili ukiwa ni pamoja na kuweka masanduku ya maoni,vibao vinanavyotoa elimu mbalimbali ikiwemo VVU/UKIMWI, ukatili na usawa wa kijinsia bila kusahau huduma ya kwanza mahala pa ujenzi" amesisitiza


Awali akisoma taarifa  ya ujenzi  Mwalimu  Mkuu wa Shule ya Msingi Bondo Oscar John   amesema, shule hiyo imepokea Tsh. mil. 110 kupitia Mradi wa BOOST kujenga madarasa 4 na matundu ya vyoo  3 ambapo ujenzi umekamilika

Ameeleza katika ujenzi huo  wamezingatia kuweka alama zote za kuonesha usalama na mazigira ya  mtoto kwa kuweka vibao vya matangazo    ili kutoa elimu kupitia  hasa usalama wa mtoto na mazingira ili watoto hao  waweze kutimiza malengo  yao.


Mwl. John ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu kwa shule hiyo sababu imesaidia kupunguza  changamoto ya elimu katika Kijiji cha Kasuku Kata ya Simbo.


Timu ya Wataalam kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Benki ya Dunia wapo kwenye ziara ya kukagua maendeleo ya miradi inayotekelezwa kupitia Mradi wa BOOST na SEQUIP.




Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)