Na. Gideon Gregory, Dodoma.
Waziri wa Katiba na Sheria balozi Dkt. Pindi Chana amewapongeza viongozi wa dini nchini kwa juhudi zao za kuendelea kupambana na vitendo vya ukatili na kuahidi kuwa,Serikali itaendelea kushirikiana nao vyema katika kuhakikisha vinatokomezwa katika maeneo yote nchini.
Dkt. Chana
ameyasema hayo leo Septemba 22,2023 Jijini Dodoma alipotembelea Ofisi za Tume
ya kurekebisha sheria Tanzania na kupokea taarifa mbili za namna Ofisi hiyo
inavyotekeleza majukumu yake.
Amesema katika
mashirikiano hayo wanapaswa kuzingatia vyema sheria na taratibu walizojiwekea
na wakishindwa kufanya hivyo watakuwa wanafanya jambo ambalo sio sawa na wale
waliopewa dhamana ya kusimamia eneo la katiba na sheria watimize wajibu wao.
“Tutaendelea kuwakumbusha watanzania, tutaendelea kutoa elimu tuzingatie taratibu fikiri sehemu ambazo mmejiwekea taratibu lakini mwingine anafanya kazi mwingine anaiba mali alizotafuta mwenzake yaani anaenda anachukua tu hiyo sio sawa, mwingine anapita tu mwingene anachukua panga anamtwanga tu hii haiwezekani tuna taratibu zetu,”amesema Dkt. Chana.
Aidha ameongeza
kuwa hawatovumilia watu wanaovunja sheria na kuvikumbusha vyombo vya ulinzi
maali popote ambapo watu hawataki kufuatia utaratibu ambao umewekwa wasisite
kutoa taarifa.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa tume ya kurekebisha sheria Tanzania Jaji Mstaafu January Msofe
amesema kuwa utafiti kluhusu makosa ya maadili ulibaini kuwa makosa hayo
yamekuwa yakiongezeka nchini ambapo mwaka 2021 jumla ya makosa 7601 ya kubaka
na kurawiti yaliripotiwa na mwaka 2022 makosa 8413 yaliripotiwa.
“Hata hivyo kesi
zinazofunguliwa mahakamani ni chache kuliko zile zinazotolewa taarifa katika
vituo vya polisi matharani katika kipindi cha 2021/22 na 2022/23 ofisi ya taifa
ya mashtaka ilifungua mahakamani kesi 2980 na 4294 mtawalia za makosa dhidi ya maadili
yakiwemo ya ukatili, kubaka, kujaribu kabaka, kurawiti, na kujaribu kurawiti,”amesema
Jaji Mstaafu Msofe.
Jaji Mstaafu Msofe ameongeza kuwa taarifa zionesha kuwa kuna kesi kubwa za makosa dhidi ya maadili ambazo hazijaripotiwa katika vyombo husika.
Naye katibu Mtendaji
wa tume hiyo Griffini Mwakapeje amesema kuwa jumla ya ripoti zilizowasilishwa
serikalini ni 56 na kuongeza kuwa katika kufanya hivyo tume inaweza kufanya uchunguzi
wa sheria yoyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuiendeleza.
“Kwa kuelekezwa na
wewe Waziri au mwanasheria mkuu wa serikali tume inaweza kutoa ushauri wa
kisheria au msaada wa kisheria pale inapobidi na inapotekeleza majuku haya tume
inaweza kufanya mashirikiano na taasisi nyingine za serikali na binafsi halafu
na kutoa taarifa zake,”amesema Mwakapeje.


