Na. Mwandishi wetu – Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuyajali makundi maalum ya vijana, Watoto, wazee na wenye ulemavu.
Mhe. Patrobas Katambi amesema hayo Septemba 6, 2023 katika Mkutano wa Maafisa Ustawi wa Jamii uliofanyika Jijini Dodoma ambapo Mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko ambaye amefungua Mkutano wa mwaka wa kiutendaji wa Maafisa hao kutoka Wizara za kisekta, Taasisi za Umma na sekta binafsi zinazotoa huduma za ustawi wa jamii nchini.
Amesema Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua umuhimu wa makundi hayo aliunda Wizara mahsusi kwa ajili kushughulikia masuala yanayohusu makundi hayo ikiwemo Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na makundi maalumu na Ofisi hiyo.
Aidha, amewasisitiza Maafisa Ustawi wa Jamii kutambua matatizo na changamoto zinazokabili makundi hayo na kuwa na uwezo wa kutatua changamoto hizo kwa kutumia rasilimali zilizopo.

