Naibu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi amesema Serikali ya Korea Kusini kupitia vyuo na taasisi zake imekuwa na ushirikiano uliowezesha hospitali kuongeza ufanisi katika utoaji huduma bora kwa wananchi.
Dkt. Magandi ameyasema hayo leo alipokutana na madaktari, wakufunzi na wanafunzi kutoka Vyuo Vikuu vya Kosin na Yonsei vya nchini Korea Kusini ambao wamembelea MNH Mloganzila kwa lengo la kujifunza na kujadiliana namna ya kuendelea kuboresha na kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya taasisi hizo.
Dkt. Magandi ameongeza kuwa kupitia ushirikiano huo, Taasisi ya Korea Foundation for Health Care imeweza kukarabati wa Wodi ya watoto wachanga chini ya siku 28 (NICU) ambapo ukarabati huo umewezesha wodi hiyo kulaza watoto 60 kwa wakati mmoja kutoka watoto 30 hapo awali.
“Pamoja na kukarabati sehemu hizi za kutolea huduma tumekuwa tukipata msaada wa vifaa tiba, pia wataalamu wetu wamepata fursa ya kujengewa uwezo ambapo mpaka sasa takribani watumishi 80 wamepata mafunzo ya muda mrefu na mfupi nchini Korea” amesema Dkt. Magandi.
Dkt. Magandi amebainisha kuwa Serikali ya Korea Kusini imekuwa ikileta wataalamu kwa lengo la kuwajengea uwezo wataalamu wetu wa ndani, ambapo hivi karibuni MNH-Mloganzila kwa kushirikiana na Daktari Bingwa kutoka nchini humo imefanikiwa kufanya upasuaji wa kupandikiza figo kwa wagonjwa watatu kwa mafanikio makubwa.
Kwa upande wake Mshauri wa Taaluma kutoka Chuo Kikuu cha Yonsei Prof. Sunjoo Kang ameupongeza uongozi wa MNH-Mloganzila kwa namna inavyoendelea kuboresha huduma za afya ndio maana kila mara wamekuwa wakivutiwa kuleta wanafunzi wao kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu.
Prof. Kang ameongeza kuwa vyuo hivyo vitaendelea kushirikiana na Mloganzila kwa kubadilishana ujuzi na uzoefu katika maeneo mbalimbali ya kibobezi kwa kuleta wataalamu wao katika hospitali hii na wataalamu wa MNH-Mloganzila kwenda katika vyuo hivyo kujifunza.
Naye, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Upasuaji Dkt. Godlove Mfuko amefafanua kuwa ziara hiyo imekuwa na manufaa kwani madaktari, wakufunzi na wanafunzi hao wametembelea maeneo mbalimbali ya kutolea huduma ambapo pia itawezesha kujadiliana namna wanavyoweza kuimarisha na kutanua wigo wa ushirikiano huo.