Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Hungary zimeainisha maeneo ya ushirikiano ambayo ni biashara na uwekezaji, elimu, utalii, uwezeshaji wa wanawake kiuchumi pamoja na majadiliano ya kidiplomasia.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Ikulu Jijini Dar es Salaam baada ya kumaliza mazungumzo na mgeni wake Rais wa Hungary Mheshimiwa Katalin Novák, Dkt. Samia amesema kuwa mazungumzo yao yamekuwa na mafanikio makubwa kwa pande zote mbili kwa kuanisha maeneo ya ushirikiano.
Rais Dkt. Samia amesema ziara ya kikazi ya Mhe. Katalin ni ya kihistoria kwa sababu imekutanisha Marais wanawake wawili ambapo kila mmoja ni wa kwanza katika nchi yake kushika wadhifa huo.
Rais Samia ameeleza kuwa Tanzania na Hungary zimekubaliana kuanzisha majadiliano ya kidiplomasia ambayo yatatoa fursa kwa pande mbili kufanya majadiliano ya mara kwa mara kuhusu maeneo mbalimbali ya ushirikiano.
Rais Dkt. Samia amesema kuwa kiwango cha biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Hungary ni kidogo na kusisitiza umuhimu wa nchi hizo kuboresha ushirikiano katika maeneo hayo. Alitoa mfano wa takwimu za mwaka 2022 zinazoonesha kuwa thamani ya miradi iliyowekezwa nchini kutoka Hungary ni Dola za Marekani milioni 4.2 tu, kiasi ambacho ni kidogo ukilinganisha na nchi nyingine za Ulaya zilizowekeza nchini.
Kwa upande wake, Rais wa Hungary, Mheshimiwa Katalin Novák amesema amekuja Tanzania kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo utaratibu wa maisha ya Watanzania na kwamba, ziara hiyo itasalia kuwa kielelezo cha kuwakutanisha Marais wawili wanawake.
Ameongeza kuwa Hungary itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo waliyoafikiana na kwamba kukutana kwao itakuwa chachu na hamasa kwa wanawake wengine duniani kufikia malengo yao kwenye taaluma zao na uongozi.
Pamoja na mambo mengine, Rais Katalin alihitimisha maelezo yake kwa kutoa mwaliko kwa Dkt. Samia kushiriki katika mkutano wa masuala ya idadi ya watu utakaofanyika mwezi Septemba 2023 na Mkutano wa Viongozi wanawake utakaofanyika mwaka 2024 nchini Hungary.