MABALOZI WAADHIMISHA SIKU YA KIMATAIFA YA NELSON MANDELA NA WATOTO WANAOUGUA SARATANI MUHIMBILI.

MUUNGANO   MEDIA
0

Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Mh. Noluthando Mayende-Malepe akiambatana na Mabalozi wa Zambia, Uturuki, Japani, Comoro, Algeria, Nigeria Uganda, Ethiopia, Somalia na DRC wametembelea wodi ya watoto wanaugua Saratani, pamoja na bweni la watoto wanaugua saratani (Ujasiri Hostel) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ili kuwafariji na maradhi hayo ikiwa ni maadhimisho ya siku ya kimataifa ya muasisi wa Taifa hilo Mzee Nelson Mandela.


Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mh. Noluthando Mayende-Malepe ameushukuru uongozi wa MNH kwa kwa mapokezi mazuri waliyoyapata pamoja na huduma bora ambazo wameona zinatolewa kwa watoto wanaougua Saratani.


Kwa upande wake Balozi wa Comoro ambaye ni kiongozi wa Mabalozi hao Mh. Dkt. Ahamada El Badaou (Dean of the Diplomatic Corps of Tanzania) amesema kuwa katika maisha yake Nelson Mandela alipenda kufanya matendo ya kibinadamu ikiwemo kujali wenye shida hivyo wameona ni vema kumuenzi kwa kusherehekea siku hii muhimu pamoja na watoto.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Mohamed Janabi amewashukuru mabalozi hao kwa kutembelea MNH na amewaalika kuleta wagonjwa kutoka nchini mwao kuja kupata matibabu ya kibingwa Muhimbili.


“Tumekuwa tukipata wagonjwa kutoka baadhi ya nchi kama Comoro, Malawi na Zambia ambao wamekuwa wanafuata matibabu Tanzania, nawaalika na wengine wa Afrika magharibi walete wagonjwa wao Tanzania ambapo kwa sasa matibabu ya kibingwa yanapatikana kwa gharama nafuu” amesema Prof. Janabi


Siku ya kimataifa ya Nelson Mandela huadhimishwa Julai 18 kila mwaka ikilenga kuenzi maisha kiongozi huyo ambapo hutoa wito kwa watu binafsi, jamii na mashirika kuchukua muda kutafakari maadili na kanuni za Mandela na kuleta matokeo chanya katika jamii zao.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)