Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Cyprian Luhemeja amekagua na kuridhishwa na utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa usafi wa Mazingira mji wa Musoma.
Ametumia nafasi ya ziara yake kutoa maelekezo kwa Mkandarasi wa mradi huo Kampuni ya China Civil Engineering Construction Cooperation (CCECC) kumaliza kazi kwa muda uliopangwa na kuwa hakutakuwa na muda wa nyongeza.
"Mpaka sasa nimeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huu, Mkandarasi haonyeshi dalili yeyote ya kutomaliza mradi kwa wakati lakini nimsisitizie kuwa hakutakua na muda wa ziada." Mhandisi Luhemeja ameeleza.
Mhandisi Luhemeja ameongeza kuwa fedha nyingi za Serikali zimewekezwa katika mradi huo hivyo ametoa rai kwa wananchi kuutunza na kuuthamini mradi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) Mhandisi Nicas Mugisha ameeleza kuwa mradi huo utakua suluhisho la uondoshaji wa majitaka mjini Musoma.
"Musoma haijawai kuwa na mradi wa majitaka, tuliwekeza zaidi katika huduma ya majisafi na salama. Sasa imebidi tuangalie namna ya kuondosha majitaka kwani takribani asilimia 80 ya majisafi yakishatumika, yanakuwa majitaka.
Mradi huu ni Muarobaini wa tatizo la majitaka mjini Musoma" alifafanua Mhandisi Mugisha
Kwa upande wake Mhandisi Gift Kimaro kutoka Kampuni ya JkW ambao ni Mkandarasi mshauri wa mradi amesema kazi inaendelea kufanyika usiku na mchana kuhakikisha utekelezaji wa mradi unakamilika kwa wakati na wananchi wanaanza kupata huduma.
Mradi wa uboreshaji wa Usafi wa Mazingira Mjini Musoma umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 36, huku ukihusisha ujenzi wa vyoo vya umma 58 katika maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa watu ikiwemo shule, ujenzi wa mabwawa ya kuchakata majitaka, vituo vya kusukuma majitaka vine (4), pamoja na mtandao wa kusafirisha majitaka kwa umbali wa Km 42.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Cyprian Luhemeja yupo katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi mkoani Mara.