MSITUMIE BODABODA KUSHIRIKIANA NA MAJAMBAZI.

MUUNGANO   MEDIA
0

Na Mwandishi Wetu - Butiama


Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Mwenyekiti wa Taifa wa Usalama Barabarani Mhe. Jumanne Sagini amewataka Maafisa Usafirishaji Nchini (bodaboda) kutotumia vyombo vyao vya usafirishaji kushirikiana na Wahalifu wakiwemo majambazi katika kutekeleza matukio ya kuhalifu.

Naibu Waziri Sagini aliyasema hayo wakati alipokutana na kuzungumza na kundi la waendesha bodaboda linalofanya kazi zao za usafirishaji  katika eneo la makutano ya Barabara ya kuelekea Mwanza, Musoma na Tarime maarufu kama zerozero.

"Msipofanya biashara hii ya halali mtaanza kukaba watu usiku. Ombi langu kwenu  msizitumie kubeba majambazi wanaokwenda kuwadhuru Watanzania wenzetu.Taarifa tulizonazo siku za karibuni baadhi ya maeneo watu wameumizwa wale majambazi walibebwa na vijana wetu wa Bodaboda. Kama wewe unasaidiana na mhalifu tutawajumuisha wote. Nisingependa Vijana wa Bodaboda kujiingiza kwenye makundi hayo."Alisema Sagini

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Sagini amelitaka Jeshi la Polisi kupitia kikosi cha usalama barabarani kuendelea kutoa elimu  kwa Maafisa Wasafirishaji (Bodaboda)  mbinu za kuwabaini na kuwatambua  Wahalifu na kuepuka mtego wa Majambazi ambao huwakodi kama watu wanaohitaji huduma ya usafiri.

Pamoja na kuzungumza na kundi hilo pia Naibu Waziri Sagini ametoa "reflector"
elfu tatu kwa ajili bodaboda hao ili kuweza kulinda usalama wao na kuweza kutambulika hususani wakati wa usiku.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)