TAASISI ZA DINI ZAKUMBUSHWA KUZINGATIA TARATIBU NA MAADILI YA USAJILI.

MUUNGANO   MEDIA
0

Na Mwandishi Wetu, Musoma.

Akizungumza wakati akimwakilisha Waziri wa Fedha Mhe. Lameck Mwigulu Nchemba katika harambee ya ujenzi wa Kanisa Katoliki la Bikira Maria Mama wa Huruma Bisumwa harambee iliyofanyika katika kanisa la Huruma ya Mungu Kigera Mjini Musoma, Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Mhe. Jumanne Sagini amewataka Viongozi wa Taasisi zote za Kidini kufanya kazi kwa mujibu wa taratibu, katiba na maadili ya usajili wa Makanisa yao badala ya kuendeleza migogoro ambayo inapelekea kukosekana kwa amani na utulivu na kupelekea baadhi kusambaratika  


"Ukiangalia hiki ambacho kinafanywa na Taasisi za Dini  katika kuwajenga watu kiimani na kiroho inasaidia hata Utawala wa Serikali kwa Wananchi ili waendelee kuwa raia wema.Hili mlilolifanya tunawatia moyo na kwa niaba ya Mgeni rasmi mliyemualika amewaungeni mkono.Tunaami fedha hizo zilizopatikana katika harambee  zitakwenda kutumika kwa kadri ya 

mipango iliyokusudiwa  na hakuna fedha itakayochepushwa" Alisema Sagini. 


Katika hatua nyingine Naibu Waziri Sagini amelipongeza Kanisa Katoliki kwa kuwa na mfumo imara wa kuwezeshana na kushirikiana jambo ambalo linafanya kanisa hilo kutokuwa na migogoro  na amezitaka Taasisi ambazo zinamigogoro kujifunza kutoka kwa wale waliofanikiwa. 

Mkuu wa Wilaya ya Musoma  Dkt. Khalfan Haule amelipongeza na kulishukuru Kanisa Katoliki kwa namna linavyoendelea kushirikiana na Serikali  mathalani katika sekta ya Elimu na Afya hii ikionesha dhahiri kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali kuwaletea Wananchi maendeleo. 


Askofu wa Jimbo  Katoliki la Musoma Michael Msonganzila   amesema kuwa anashukuru kwa ushirikiano ambao umeendelea kuwepo kati ya Taasisi za Kidini pamoja na Serikali kwani lengo la huduma zinazotolewa ni katika kumuhudumia mwanadamu ambaye ameumbwa kimwili na kupewa roho. 


"Lengo la Taasisi yetu ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na ustawi wa Mwanadamu ikiwa ni katika roho na mwili.Tuendelee kushikamana katika makundi mbalimbali kwani ni matumaini yetu Bisumwa pale ambapo panajengwa kanisa ni matumaini yetu kuwa lazima siku moja itakuwa Parokia.Lengo ni kuendelea kusogeza huduma kwa waumini."Alisema Askofu 

Katika harambee hiyo jumla ya Shilingi milioni ishirini na tano laki nane zimechangishwa, kati ya hizo milioni kumi ikiwa ni mchango wa Mhe. Lameck Mwigulu Nchemba Waziri wa Fedha, ahadi zikiwa ni shilingi milioni tano, saruji mifuko mia moja na lori moja la mchanga tani kumi.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)