Na Mwandishi Wetu - Butiama
Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Mwenyekiti wa Taifa wa Kamati ya Usalama Barabarani Mhe. Jumanne Sagini amelitaka Jeshi la Polisi kuendelea kutoa elimu kwa Maafisa Usafirishaji (Bodaboda ) ili kuweza kuwabaini abiria ambao huwa wanawakodi wakiwa na lengo la kutekeleza uhalifu ikiwemo ujambazi.
Naibu Waziri Sagini aliyasema hayo wakati alipokutana na kuzungumza na kundi la waendesha bodaboda linalofanya kazi zao za usafirishaji katika eneo la makutano ya Barabara ya kuelekea Mwanza, Musoma na Tarime na Sirari maarufu kama zerozero.
"Msipofanya biashara hii ya halali mtaanza kukaba watu usiku. Ombi langu kwenu msizitumie kubeba majambazi wanaokwenda kuwadhuru Watanzania wenzetu.Taarifa tulizonazo siku za karibuni baadhi ya maeneo watu wameumizwa wale majambazi walibebwa na vijana wetu wa Bodaboda. Kama wewe unasaidiana na mhalifu tutawajumuisha wote. Nisingependa Vijana wa Bodaboda kujiingiza kwenye makundi hayo.Jeshi la Polisi kupitia kikosi cha Usalama Barabarani litaendelea kuandaa mafunzo na kutoa mafunzo ya kiusalama juu ya namna ya kuwatambua watu wanaowakodi wakiwa na dhamira ya kutekeleza uhalifu katika maeneo mbalimbali" alisema Sagini
Naibu Waziri Sagini amewasisitiza bodaboda kuendelea kufuata sheria za usalama barabarani na kuwaunga mkono katika kulinda usalama wao kwa kuwapatia "reflector" elfu tatu kwa ajili ya kuwasaidia kuonekana wakati wa usiku.




