Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Adolf Ndunguru amewaagiza Makatibu Tawala wa Mikoa(MA-RAS) kuhakikisha zinaingizwa benki Sh. Bilioni 1.6 ambazo zilikusanywa na baadhi ya Halmashauri kwenye maeneo hayo wakati wa kufunga mwaka wa fedha 2022/23.
Ndunguru ameyasema hayo leo Julai 04, 2023 jijini Dodoma alipokuwa akifunga kikao kazi cha siku mbili cha kutambua mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa Programu ya Mifumo katika Sekta ya Umma kwa baadhi ya Watendaji wa Mikoa.
Amesema kwa mwaka wa fedha 2022/23 ambao tayari umeisha Juni 30, 2023 bado zipo baadhi ya Halmashauri ambazo hazijamaliza kazi ya usuluhishi wa mahesabu yake na baadhi ya Halmashauri bado zimeendelea kubaki na fedha mbichi kiasi cha Sh. Bilioni 1.6
“Tumebaini bado kuna Halmashauri zimeendelea kubaki na fedha mbichi, tunapofunga mwaka tuna takribani Sh.Bilioni 1.6 hazijapelekwa benki bado mnazo mikononi, nawasihi muende mkawasimamie Wakurugenzi wahakikishe kwamba fedha hizo kwanza wakamilishe usuluhishi wa mahesabu, lakini wahakikishe fedha hizo mbichi ambazo bado wanazo mikononi zinakwenda benki,” alisema Ndunguru.
Aidha, amewasihi Viongozi hao kuwa katika mwaka wa fedha uliopita 2022/2023 kulikuwa na Hati chafu moja na hivyo wahakikishe katika mwaka huu isiwepo hati chafu hata moja kwani hakuna sababu ya kuwa na hati chafu.
Katika hatua nyingine, akihitimisha kikao hicho, Katibu Mkuu Ndunguru amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendelea kutoa ushirikiano wa hali juu kwa Mradi wa PS3+ ili kuendeleza na kuimarisha Mifumo na miundombinu ya TEHAMA kwenye Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi zilizo chini yake pamoja na vituo vya kutolea huduma ya afya ya msingi na elimu ili kuongeza ufanisi, uwajibikaji na utoaji huduma bora kwa wananchi ili kufikia azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kikao kazi hicho kimepitia dhana nzima ya kutaasisisha Mifumo ya TEHAMA Serikalini kwa kubainisha majukumu ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na kupata ufafanuzi wa maeneo ambayo yanahitaji maboresho kama vile ushirikishwaji wa sehemu zote katika uratibu na utekelezaji Mifumo Serikalini kupitia Mradi wa PS3+.