DAR ES SALAAM.
Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi(UV CCM) umesema ushirikiano kati ya DP world na serikali umejikita zaidi katika kuboresha uendeshaji wa bandari nchini na kuongeza tija na ufanisi.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam Mwenyekiti wa Uv CCM Taifa Mohamed Kawaida amesema kinachofanyika siyo kitu alichoamua mtu binafsi bali ni maelekezo ya Chama kupitia ilani yake ya uchafuzi mwaka 2020/2025 na ndiyo inayounganisha moja kwa moja na Serikali iliyopo madarakani.
“Ni kweli kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeingia mkataba wa Mashirikiano na Serikali ya Dubai kwa kuanzisha ushirikiano wa kuboresha, kuendesha na kuendeleza maeneo ya Bandari nchini,” amesema Kawaida.
Aidha amesema kuwa jitihada zote na hatua ambazo zinachukuliwa na Serikali ya Awamu ya sita katika kuvutia uwekeza nchini hususani kwenye maeneo ya bandari nchini zinalenga kumalizia changamoto za muda mrefu ikiwemo ucheleweshwaji wa meli mizigo na kukosekana kwa ufanisi katika bandari zetu ambako kumekuwa kukichangia katika sekta zingine .
Hata Hivyo amebainisha kuwa majadiliano na Maandalizi ya mkataba huo yamefanywa na timu ya wataalam wa Tanzania ambao wana uzoefu mkubwa katika masuala ya mikataba ya kimataifa na kabla ya kusainiwa ikizingatia taratibu zote za Nchi.