SIMBA YAUNGA MKONO ‘FIGO MARATHON’.

MUUNGANO   MEDIA
0

 


Klabu ya soka ya Simba (Simba Sports Club) itashirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga na Mloganzila pamoja na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Heathier Kidney Foundation katika kufanikisha mbio za ‘Figo Marathon’ zinazotarajiwa kufanyika Julai 9, mwaka huu katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam. 


Hayo yamesemwa leo na Msemaji wa klabu hiyo Bw. Ahmed Ally wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga na kuongeza kuwa klabu hiyo imekuwa ikishiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii.


Mbio hizo zinalenga kukusanya fedha kwa ajili ya kusaidia wagonjwa wenye matatizo ya figo na kuwasihi washabiki, wanachama wa Simba na wananchi kwa ujumla kushiriki katika mbio hizo ambazo zinalenga kuisaidia jamii.



“Wapo wananchi wengi wanakabiliwa na matatizo ya figo wakiwemo washabiki na wanachama wa simba hivyo ni wajibu wetu sote kujitokeza kwa wingi katika kuunga mkono mbio hizi ambazo zinalenga kuwasaidia watanzania wenzetu” amesema Bw. Ally


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amesema ipo haja ya jamii kuunganisha nguvu katika kuiunga mkono serikali katika matibabu ya magonjwa ya figo kwa kuwa matibabu yake yanahitaji gharama kubwa.


Prof. Janabi ameongeza kuwa tatizo la ugonjwa wa figo ni kubwa ambapo MNH (Upanga na Mloganzila) inahudumia wagonjwa wanaohitaji huduma za kuchuja damu kwa wagonjwa 130 hadi 150 kwa siku na kusisistiza kuwa suluhisho la kudumu la matibabu ya figo ni upandikizaji.

Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo, Dkt. Jonathan ameongeza kuwa hospitali inaendelea kutoa elimu kwa jamii namna ya kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwa ni pamoja na kubali mtindo wa maisha kwa kula vyakula kulingana na ushauri kutoka kwa wataalam wa lishe na kufanya mazoezi na kuepuka tabia za kukaa bwete.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)