WANANCHI KIJIJI CHA MAJALILA WAISHUKURU SERIKALI KUWAJENGEA SHULE.

MUUNGANO   MEDIA
0


 Asila Twaha - Katavi, Tanganyika

Wananchi Kijiji cha Majalila Kata ya Tonge Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi wameishukuru Serikali kwa kujenga Shule ya Sekondari Majalila  ambayo imewapunguzia adha watoto wa eneo hilo  kutembea umbali  mrefu  kufuata elimu.


Akiongea kwa  niaba ya wananchi Mwenyekiti wa Kijiji cha Majalila Bw. Ally Chuma amesema kukamilika kwa shule hiyo kumewasaidia  wanafunzi hao   kupunguza  kutembea umbali mrefu kufuata huduma na  gharama  za usafiri kwa wazazi.


Ameendelea kufafanua kuwa  kukamilika kwa shule hiyo kumepunguza  mrundikano wa  wanafunzi.


“Kwakweli tulipoambiwa tunajengewa shule katika kata yetu tulishirikiana na wananchi wangu na  tulifurahishwa sana na tulishirikiana kusafisha eneo  lililojengwa shule hii na kusaidia shughuli  nyengine ili shule ikamilike haraka” amesisitiza

Kwa upande wa Afisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mwl. Roza Nabahani amesema Halmashuri hiyo ilipokea sh. milioni 470 kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) kujenga shule hiyo ya Sekondari kwenye  maeneo yaliyo na changamoto ya ukosefu wa shule ya sekondari.


Amesema Halmashauri kwa kushirikiana na wanakijiji walihakikisha eneo linapatikana  na kufuata  maelekezo yote  yaliyotolewa na Serikali  yalifuatwa.


“shule asilimia kubwa imekamilika na tumeshaisajili na sasa wanafunzi wameshaanza kusoma na wanaendelea na masomo yao na walimu wanaendelea na majukumu yao hivyo shule hii ni mkombozi mkubwa katika eneo hili sababu itasaidia mpaka kata za jirani” amesema Nabahani


Naye  Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Majalila Jidala Deus amesema  hivi sasa wanauwezo wa kufikia   malengo yao kwasababu hakuna vikwazo  vinavyoweza kuwasababishia kutokumaliza shule kwa kuwa shule hiyo imejengwa karibu na maeneo wanayoishi na inawasaidia  kupata muda mwingi wa kujisomea.


Bi. Scolastika Mayene(mzazi) ameishukuru Serikali  kwa kuwajengea shule katika kata yao kwa kuwa wazazi wengi itawasadia kwa kuwapunguzia gharama ya nauli

na itasaidia kuongeza ushirikiano kati yao wazazi  na walimu kwa ukaribu.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)