Na Gideon Gregory, Dodoma.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa pamoja na kuimarisha huduma za tiba hapa nchini, serikali imejipanga kuweka jitihada za kipekee ili kuzuia na kudhibiti ugonjwa wa shinikizo la juu la damu na magonjwa yasiyoambukiza.
Waziri Ummy ameyasema hayo leo Mei 17,2023 Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni maadhimisho ya siku ya shinikizo la damu Duniani.
Amekumbusha umuhimu wa kubadili mtindo wa maisha na kuhimiza wananchi kufanyaji wa mazoezi, kuepuka tabia bwete, kuepuka matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, kupunguza matumizi ya vilevi, kuzingatia ulaji unaofaa wa mlo kamili wenye mboga mboga na matunda ya kutosha ili kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya magonjwa.
Aidha, amesema kuwa takwimu kutoka kwenye mfumo wa ukusanyaji taarifa za Afya (DHIS2) zinaonesha kuwa jumla ya wagonjwa 2,535,281 walitibiwa magonjwa yasiyoambukizwa kwenye vituo vya Afya nchini kwa mwaka 2017.
“Wagonjwa hawa wameongezeka hadi kufikia wagonjwa 3,440,708 kwa mwaka 2021 ongezeko hili (la wako 905,427 kwa kipindi cha miaka mitano, ni sawa na ongezeko la asilimia 9.4%,”amesema.
Waziri Ummy amesema kati yao, ugonjwa wa shinikizo la juu la damu ndio uliongoza miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza ambapo waliongezeka kutoka wagonjwa 688,901 kwa mwaka 2017, hadi kufikia wagonjwa 1,345,847 kwa mwaka 2021 sawa na ongezeko la 95.4% katika kipindi hicho.
“Takwimu hizi zinatuonesha kwamba wagonjwa hawa wenye shinikizo la damu wameonekana kuongezeka takribani mara mbili zaidi kwa kipindi cha miaka mitano (Health Statistical Bulletin 2022),”amesema.
Vilevile ameongeza kuwa, kwa wagonjwa waliotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) tangu ilipoanzishwa Septemba 2015 hadi Aprili 2023 kati ya wagonjwa 619,102 tuliowatibu asilimia 66 ya wagonjwa walikuwa na tatizo la ugonjwa wa shinikizo la juu la damu.
“Hii inamaanisha kuwa kwa kila wagonjwa 10 wanaoonwa JKCI, wagonjwa 6 wana ugonjwa wa shinikizo la juu la damu,”ameongeza.
Amesema katika uchunguzi uliofanywa katika jamii kwenye mikoa ya Pwani, Arusha, Geita, Mtwara, Lindi, Zanzibar, Iringa na Dar es Salaam takwimu zinaonyesha watu 3-4 kati ya 10 wana shinikizo la juu la damu.
“Shinikizo la juu la damu ndilo sababu kubwa (vihatarishi) la kiharusi (stroke), shambulio la moyo (Heart attack), moyo kushindwa kufanya kazi (Heart Failure), kutuna kwa kuta za mishipa ya damu, moyo, uharibifu kwenye chujio za figo, ganzi miguuni na mikononi, upofu na kupunguza nguvu za kiume,”amesema.
Shinikizo la juu la damu ni ugonjwa unaosababishwa na nguvu ya msukumo wa damu katika mishipa kuwa kubwa kuliko kawaida kwa muda mrefu na ongezeko hilo huulazimu moyo kufanya kazi kupita kiasi ili uweze kusukuma damu katika mishipa kwa kiwango kilekile kinachohitajika mwilini.
Kila mwaka ifikapo Mei 17 Dunia huadhimisha siku ya Shinikizo la Juu la Damu ambapo mwaka huu kauli mbiu inasema “Pima Shinikizo la Damu Kwa Usahihi, Idhibiti, Ishi kwa Muda Mrefu” inayolenga kuongeza utambuzi sahihi wa shinikizo la damu ulimwenguni kote, haswa katika nchi zenye kipato cha kati na cha chini ili kuwahamasisha wananchi kujitokeza kupima shinikizo la damu mapema.