TLS NA KAMATI YA MAWAKILI KUCHUKUA HATUA KALI ZA KINIDHAMU NA KISHERIA.

MUUNGANO   MEDIA
0

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Chama Cha Mawakili Tanganyika (TLS) na Kamati ya Mawakili kuchukua hatua kali za kinidhamu na kisheria dhidi ya mawakili wachache wanaoharibu heshima ya taaluma ya sheria kwa kukosa uadilifu na maadili mema.


Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 11 Mei 2023 wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC). Amesema kumekuwa na tuhuma kwa baadhi ya Mawakili kujihusisha na vitendo vya rushwa na udanganyifu kwa maslahi yao binafsi ikiwemo kuwasaliti wateja kwa kupokea rushwa kutoka upande wa pili na kuharibu kesi.

 

Makamu wa Rais ametoa rai kwa TLS kuhakikisha inashirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria kutoa elimu kwa umma kuhusu suala la mihuri ya kielektroniki ili kuondokana na suala la vishoka na mawakili wanaotumia mihuri isiyo halali kufanya kazi za uwakili. Pia ameziagiza taasisi zote za serikali pamoja na taasisi binafsi kuhakikisha zinatumia mihuri ya kielektroniki ili kuondokana na kadhia hiyo.

 


Halikadhalika Makamu wa Rais amesema ni wajibu wa sekta na taasisi za sheria kuendelea kuchambua, kubaini na kutoa mapendekezo ya sheria zinazotakiwa kufanyiwa marekebisho au kuandikwa upya hapa nchini. Amesema ni vema kuweka nguvu zaidi katika kutoa elimu ya sheria kupitia mihadhara, redio, televisheni na mitandao ya kijamii ili kuondoa adha ya watu wengi wanaopoteza haki zao kwa kukosa uelewa wa sheria. Ametoa rai kwa mawakili wasomi wote nchini, pamoja na taasisi husika, kuendelea na moyo wa kurejesha kwa jamii kwa kujitolea kuwasaidia wananchi wasio na uwezo wa kulipia gharama za kesi mahakamani.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)