Na Emmanuel Kawau.
Wakala wa majengo Tanzania (TBA) hii leo Mei 8/2023 wametangaza rasmi kuongezwa muda wa manunuzi kwa wakaazi wa Magomeni Kota kutoka miaka kumi na tano (15) iliyoelekezwa na Serikali awali hadi kuwa miaka thelathini (30) ikijumuisha miaka mitano (5) ya kukaa bure.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mapema hii leo ofisini kwake Jijini Dar es salaam Mtendaji Mkuu Wa TBA, Arch Daud Kondoro amesema Baada ya timu ya wataalam kufanya tathmini kwa kuzingatia maelekezo ya Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu,gharama za ununuzi wanyumba hizo ni Milioni 48,522,913. kwa nyumba ya chumba kimoja na Milioni 56,893,455. Kwa nyumba ya vyumba viwili.
"Hatahivyo baada ya waakazi wa Magomeni Kota kujulishwa juu ya gharama hizo,wakaazi walimuomba Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwapunguzia gharama za
ununuziwa nyumba hizo pamoja na kuwaongezea muda wa kulipia".
"Baada ya kupokea maombi hayo, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameridhia kuwaongezea muda wa manunuzi, wakaazi wa Magomeni Kota kutoka miaka kumi na tano(15) iliyoelekezwa na Serikali awali hadi kuwa miaka thelathini (30) ikijumuisha miaka mitano (5) ya kukaa bure" Amesema Kondoro.
Aidha amesema Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) iko tayari kuwatambua wakaazi waliotayari kutekeleza utaratibu huo wa ulipaji na kuingia nao mkataba wa mkaazi mnunuzi, Pia TBA iko tayari kuwatambua wakaazi wasiokuwa tayari kutekeleza utaratibu huu ambao wataruhusiwa kukaa bure kwa miaka mitano (5) na baada ya muda huo kukamilika, nyumba watazirejesha kwa
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).