MAHAKAMA ya Mwanzo Wilaya ya Kongwa, Mkoa wa Dodoma imemuhukumu kifungo cha miezi 12, Ernest Koti na kulipa faini ya Sh 6 Milioni kwa kosa la wizi wa miundombinu ya maji.
Hukumu hiyo imetolewa Mei 02, 2023 na Hakimu Mkazi Renada Mkangala baada ya mshtakiwa kukiri kosa kuwa ni kweli alikuwa akichimba mabomba ambayo ni mali ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA).
Hakimu alisema kutokana na mshtakiwa kukiri kosa Mahakama inamtia hatiani chini ya kifungu cha 37 (1) cha jedwali la tatu sheria ya Mahakama ya Mahakimu sura ya 11 mapitio ya mwaka 2019 kosa moja la wizi.
“Kutokana na mshtakiwa kukiri kosa kuwa kweli, vilevile mshtakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza, mahakama imeona mshtakiwa atumikie kifungo cha miezi 12,” alisema Hakimu
Hakimu Mkangala alisema rufaa ipo wazi kwa pande zote kwa asiyeridhika na hukumu hiyo ndani ya siku 30.