ASILIMIA 98.6 YA WATOTO NCHINI WAMECHANJWA CHANJO YA PENTA3 – WAZIRI UMMY.

MUUNGANO   MEDIA
0

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Waziri wa Afya Mh. Ummy Mwalimu amesema kuwa serikali imeendelea kusimamia na kuimarisha huduma za kinga ikiwemo kuhakikisha chanjo na vifaa vya kutolea chanjo vinapatikana kulingana na mahitaji ya Mikoa yote nchini. 

Waziri Ummy ameyasema hayo leo Mei 12,2023 wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara Bungeni Jijini Dodoma, ambapo amesema lengo la kutoa chanjo hizo ni kuhakikisha kuwa watoto wote wenye umri chini ya mwaka mmoja, wajawazito na wasichana wenye umri wa miaka 14 ambao ni walengwa wa huduma za chanjo wanapata huduma hizo kwa wakati.

Amesema Wizara imeendelea kuhakikisha chanjo za watoto wadogo za kuwakinga na magonjwa ikiwemo Pepopunda, Kifaduro, Kupooza, Surua, Homa ya Uti wa Mgongo, Kifua Kikuu, Dondakoo, Nimonia, Homa ya Ini, Rubella na Kuharisha zinapatikana bure kulingana na mahitaji. 

“Katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023, Wizara ilinunua dozi 2,186,800 za IPV (Inactivated Polio Vaccine) kwa ajili ya kuzuia ugonjwa wa Kupooza kwa Watoto, Chanjo ya Pentavalent dozi 1,763,500 kwa ajili ya kuwakinga watoto dhidi ya Kifaduro, Dondakoo, Kupooza, Homa ya Ini na Homa ya Uti wa Mgongo, Chanjo ya Pneumococal Conjugate Vaccine (PCV) dozi 4,290,800 kwa ajili ya kuwakinga watoto dhidi ya Homa ya Mapafu (Nimonia) na Homa ya Uti wa Mgongo, Chanjo ya Bivalent Oral Polio Vaccine (BOPV) dozi 7,263,000 kwa ajili ya kuzuia virusi mbalimbali vinavyosababisha ugonjwa wa Kupooza kwa watoto, Chanjo ya Rotarix (Rota) dozi 3,656,000 kwa ajili ya kuwakinga watoto dhidi ya kuhara kukali, Chanjo ya Surua na Rubella (MR) dozi 3,195,000 kwa ajili ya kukinga watoto na ugonjwa wa Surua na Rubella, Chanjo ya Bacillus Calmette Geurin (BCG) dozi 5,900,000 kwa ajili ya kuwakinga watoto wachanga na ugonjwa wa Kifua Kikuu; na Chanjo za kampeni ya Polio dozi 17,761,880,”amesema.

Aidha, amesema Chanjo hizo ni nyongeza ya dozi za chanjo ambazo zilikuwepo tayari katika maghala ya dawa, ambazo zilikuwa ni IPV dozi 2,186,800, Pentavalent dozi 1,763,500, PCV dozi 1,376,000, bOPV dozi 7,263,000, Rota dozi 3,576,000, MR dozi 1,960,000; BCG dozi 12 3,978,980, na HPV dozi 1,084,540 ambapo Chanjo zote zilizoagizwa zilipokelewa na kusambazwa kwenye mikoa yote kulingana na idadi ya walengwa na uhitaji.

Amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha wa kuanzia Julai 2022 mpaka Machi 2023, Wizara ya Afya ilikuwa na lengo la kuchanja jumla ya watoto 1,618,737 hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu jumla ya watoto 1,596,951 sawa na asilimia 98.6 walikuwa wamechanjwa chanjo ya Penta3 ambayo hutumika kama kipimo kikuu cha chanjo ikiwa ni ongezeko la asilimia 4 ikilinganishwa na uchanjaji wa kipindi kama hicho mwaka 2021/22.

“Uchanjaji wa chanjo ya Surua na Rubella dozi ya kwanza ulifikia asilimia 98.1 ikilinganishwa na asilimia 95 kwa kipindi kama hicho mwaka 2021/22; Surua na Rubella dozi ya pili ilifikia asilimia 96.7 ikilinganishwa na asilimia 84 kwa kipindi kama hicho mwaka 2021/22, huduma za chanjo ya kuwakinga watoto dhidi ya ugonjwa wa Polio, kwa kutumia chanjo ya matone (OPV3) ulifikia asilimia 99.2 ikilinganishwa na asilimia 98 kwa kipindi kama hicho mwaka 2021/22, uchanjaji kwa kutumia sindano (IPV) ulifikia asilimia 100 ikilinganishwa na asilimia 98 kwa kipindi kama hicho mwaka 2021/22. Juhudi hizi zinalenga kuhakikisha kuwa tunazuia ugonjwa wa Polio hapa nchini,”ameongeza.

Sanjari na hayo amesema pamoja na utekelezaji wa utoaji wa chanjo kulingana na miongozo, Wizara kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo ya afya, imetekeleza kampeni mbalimbali za utoaji wa chanjo kwa Watoto ikiwemo kudhibiti Polio na kampeni ya chanjo ya Surua.

“Kwa upande wa chanjo ya Polio, awamu ya kwanza ilifanyika katika mikoa minne inayopakana na nchi ya Malawi ambayo ni Mbeya, Njombe, Ruvuma na Songwe ambapo ililenga kuwafikia watoto 975,839. Katika awamu hiyo watoto 1,130,261 walifikiwa sawa na asilimia 115.8. Awamu ya pili ilifanyika katika mikoa yote nchini ikilenga kuwafikia watoto 10,576,805 ambapo watoto 12,436,361 sawa na asilimia 117.58 walifikiwa. Awamu ya tatu ililenga kuwafikia watoto 12,692,166 ambapo watoto 15,052,442 sawa na asilimia 118.6 walifikiwa, na awamu ya nne ililenga kuwafikia watoto 15,052,442 ambapo watoto 17,816,933 sawa na asilimia 118.8 walifikiwa,”amesema.

Pia amesema Wizara imekadiria kutumia zaidi ya Trilioni 1 ambazo zitakazotumika kutekeleza majukumu ya Wizara ikiwa ni pamoja na uendeshaji wa Ofisi na miradi ya maendeleo nchini.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)