WAZIRI MASAUNI AKOSHWA NA UJENZI VITUO VYA ZIMAMOTO NCHINI, AMSHUKURU RAIS SAMIA KURIDHIA KUTOA FEDHA.

MUUNGANO   MEDIA
0

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya kisasa vya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini ambavyo vitasaidia kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

Waziri Masauni ameyasema hayo jijini Dodo.a, leo Jumatano Aprili 26, 2023 wakati hafla ya ufunguzi wa vituo vya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji vya Nzuguni na Chamwino.

Amesema uzinduzi wa vituo hivyo ni sehemu ya miradi inayozinduliwa katika juma la kilele cha maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Vituo hivyo vilivyozinduliwa leo na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa vimegharimu zaidi ya shilingi Bilioni 2.3.

“Serikali ya awamu ya sita katika kipindi hiki tutashuhudia mapinduzi makubwa ya ununuzi wa vifaa ndani ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika kufanikisha hilo tayari mchakato upo katika hatua za mwisho, tumejipanga kununua hadi helikopta za kuzimia moto,” alisema Masauni.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, CGF John Masunga amesema Serikali imeendelea kutatua changamoto za jeshi hilo ikiwemo kununua boti za uokoaji majini, na pia kuwezesha kupatikana kwa mkopo wa masharti nafuu wa Euro milioni 4.9 kutoka Serikali ya Austria kwa ajili ya ununuzi wa magari 12 ya kuzima moto yakiwamo magari mawili yenye ngazi kwa ajili ya majengo marefu hapa nchini.

CGF Masunga ameongeza kuwa Serikali imeliwezesha Jeshi hilo kukamilisha ujenzi wa Kituo Kikuu cha Jeshi hilo Manispaa yaTemeke Jijini Dar es Salaam.

Ameongeza kuwa Serikali pia inatekeleza Mpango wa kuisaidia zaidi Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kupata Vitendea kazi vya Dola za Marekani milioni 100 ambapo itatua kwa kiasi kikubwa ukosefu wa vitendea kazi.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)