Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama wametoa wito kwa watumishi wa umma nchini kila mmoja kwa nafasi yake kufanya kazi kwa bidii, uadilifu, ubunifu na ushirikiano ili kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutekeleza azma yake ya kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mhe. Simbachawene na Mhe. Jenista wametoa wito huo kwa watumishi wa umma, wakati wa hafla ya makabidhiano ya ofisi, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) jijini Dodoma ikiwa ni siku chache tangu wateuliwe na kuapishwa tarehe 02 Aprili, 2023 Ikulu Jijini Dar es Salaam na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kushika nyadhifa walizonazo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo ya ofisi, Mhe. Simbachawene amewataka watumishi wa umma kuendelea kuchapa kazi ili kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuujenga utumishi wa umma unaowajibika kwa kutoa huduma bora kwa wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zitolewazo na taasisi za umma.
Mhe. Simbachawene amesema, ili taifa lipate maendeleo ni lazima kila Mtanzania anayepata nafasi kuhakikisha anaitendea haki kwa kuwa mbunifu na kuchapa kazi ili kufikia maono ya viongozi wakuu wa nchi ambao wamedhamiria kuliletea taifa maendeleo.
“Viongozi wetu wakuu wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wanabeba maono yenye ndoto za mafanikio, hivyo tunapaswa kutafsiri na kuziishi ndoto zao kwa matendo ili mwisho wa siku tutoe huduma bora kwa Watanzania pamoja na kutoa mchango katika maendeleo ya taifa,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.
Aidha, Mhe. Simbachawene ameahidi kumpa ushirikiano wa kiutendaji Mhe. Jenista Mhagama ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwataka kumsaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.


