
Ukosefu wa uhakika wa chakula unaelekea kufikia kiwango cha juu zaidi katika miaka 10 katika Afrika Magharibi na Kati ifikapo Juni.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa imetahadharisha kuhusu "kupanuka kwa wasiwasi" wa ukosefu wa chakula katika nchi za ukanda wa Sahel na viwango vya janga la njaa hasa katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro ya Burkina Faso na Mali ambako utoaji misaada ya kibinadamu unatatizwa pakubwa na ukosefu wa usalama.
Ripoti hiyo ilibaini kuwa, athari za pamoja za migogoro, majanga ya tabianchi, COVID-19 na bei ya juu ya vyakula zinaendelea kuzidisha njaa na utapiamlo katika eneo hilo."
Idadi ya watu ambao mara kwa mara hukumbwa na tatizo la uhaba wa chakula salama na chenye lishe bora inatarajiwa kufikia milioni 48 katika msimu wa kuanzia Juni hadi Agosti 2023 ikiwa ni ongezeko mara nne katika miaka mitano iliyopita.
Ripoti hiyo imetabiri kuwa kutakuwa na upanuzi wa kijiografia wa ukosefu wa chakula katika eneo hilo.
Huku hali mbaya ya usalama ikizidi kuongezeka kwa viwango hatari hatari, Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Magharibi wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Chris Nikoi amesema "hali mbaya ya usalama wa chakula na lishe katika Afrika Magharibi inasikitisha.
Amesema ni muhimu kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika kujenga uwezo wa jamii na watu binafsi kuhimili mishtuko, huku kipaumbele kikitolewa kwa ufumbuzi wa ndani na wa muda mrefu wa uzalishaji wa chakula.
Hivi karibuni ripoti mpya iliyochapishwa na taasisi moja inayofuatilia mashambulizi na mienendo ya makundi ya kigaidi duniani ilisema kuwa, vifo vinavyotokana na hujuma za kigaidi katika eneo la Sahel barani Afrika vimeongezeka kwa asilimia 2000 katika kipindi cha miaka 15 iliyopita.
Ripoti hiyo iliyochapishwa na taasisi ya Institute for Economics and Peace yenye makao yake Australia imeeleza kuwa, eneo la Sahel katika chini ya jangwa la Sahara barani Afrika ndicho kitovu cha ugaidi hivi sasa duniani.
Chanzo #Parstoday