Zaidi ya nusu ya Waingereza wanapinga kutumika pesa za walipa kodi nchini humo kufadhili sherehe ya kutawazwa Mfalme Charles III wakati huu nchi hiyo ikikabiliana na mfumuko wa bei uliovunja rekodi na mgogoro wa gharama kubwa ya maisha.
Hayo ni kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliofanywa na kampuni ya utafiti ya YouGov yenye makao yake makuu London, na kuchapishwa Jumanne. Uchunguzi huo unaonyesha kuwa, asilimia 51 ya waliohojiwa walionyesha kupinga kutumika fedha za serikali kufadhili sherehe ya Mei 6 ta kutawazwa Mfalme Charles na mke wake, Camilla.
Ni asilimia 32 pekee ya watu wazima 4,246 walioshiriki katika kura hiyo ya maoni walipendelea serikali ifadhili sherehe hiyo ya gharama kubwa huku asilimia 18 wakijizuia kutoa maoni.
Takriban asilimia 62 ya waliohojiwa wenye umri wa miaka 18 hadi 24 walionyesha kupinga ufadhili wa serikali katika kutawazwa Charles na ni asilimia 15 pekee waliunga mkono hatua hiyo.
Sherehe ya kutawazwa kwa mfalme huyo mwenye umri wa miaka 74 imepangwa kufanyika Mei 6, licha ya kuendelea kwa mfumuko wa bei nchini humo na mgogoro mkubwa wa kupanda gharama ya maisha ambao haujawahi kushuhudiwa nchini humo.
Serikali, wakati huo huo, bado haijafichua ni kiasi gani itagharimu kufanya sherehe ya kutawazwa Charles inayojumuisha msafara rasmi wa kifalme, tamasha katika Windsor Castle, karamu za mitaani n.k. Wataalamu wa masuala ya kifedha wanasema sherehe hiyo inatarajiwa kugharimu makumi ya mamilioni ya pauni.
Kasri ya Buckingham imesema sherehe ya kutawaza Charles itafanyika kuanzia Mei 6-8.
Hayo yanajiri wakati Uingereza hivi karibuni imekuwa ikipambana na kupanda kwa gharama za maisha, kupanda kwa mfumuko wa bei, kupanda kwa gharama za mafuta, na migomo ya wafanyakazi wa sekta mbali mbali wanaotaka nyongeza ya mishahara. Ongezeko la mfumuko wa bei Uingereza linakua kwa kasi zaidi kuliko wastani wa ongezeko la mishahara nchini kote.
Mzozo wa Ukraine na shida ya nishati iliyoibuliwa na mzozo huo na vile vile uchumi ambao bado umeathiriwa na janga la corona ni kati ya sababu kuu zinazosababisha matatizo ya kiuchumi Uingereza.
Pamoja na matatizo hayo yote, serikali ya Uingereza ni miongoni mwa waungaji mkono wakubwa wa serikali ya Ukraine katika vita vyake dhidi ya Russia, ambapo imeipa serikali ya Kiev misaada ya kijeshi yenye thamani ya mabilioni ya pauni.