MAPIGANO YAENDELEA SUDAN, HUKU VIFAA VIKIPUNGUA HOSPITALINI.

MUUNGANO   MEDIA
0



Mapigano makali yanaripotiwa kuendelea nchini Sudan baina ya majenerali hasimu huku Mkuu wa Shirika la Afya Duniani akitoa wito kwa pande zote katika mzozo nchini humo kuwezesha vituo vya matibabu kuwahudumia wale wote wanaohitaji huduma. Aidha ameonya kuhusu kuanza kupungua vifaa vya matibabu na wafanyikazi wa ya afya katika mji mkuu Khartoum wakati mapingano yanashadidi.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus ameonya kuhusu mzozo wa kibinadamu nchini humo, ikiwa ni pamoja na kukaribia kuporomoka kwa mfumo wa afya.

Tedros alisema baadhi ya hospitali tayari zimefungwa au ziko ukingoni kwa sababu ya mashambulizi na ukosefu wa wafanyakazi na vifaa vya matibabu. Baadhi ya vituo vya afya viliripotiwa kuporwa na vingine vikitumika kwa madhumuni ya kijeshi, alisema.

Vifaa vilivyosambazwa kwa vituo vya afya kabla ya kuongezeka kwa mzozo hivi karibuni vilimalizika na hospitali katika mji mkuu Khartoum zilikuwa zikiripoti uhaba wa wafanyakazi na vifaa vya matibabu vya kuokoa maisha, alisema.

Hadi sasa waliofariki katika mapigano ya siku tano Sudan wamefika wamefika 270 huku  waliojeruhiwa wakizidi 2,600.

Mapigano ya kuwania madaraka ni baina Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, kamanda wa vikosi vya jeshi ambaye pia ni mtawala wa Sudan, na  Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, mkuu Vikosi vya Msaada wa Dharura (RSF). Majenerali hao wawili ni washirika wa zamani kwani walishirikiana kutekeleza  mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba 2021.

Ghasia hizo zimeibua wasiwasi wa vita vya wenyewe kwa wenyewe wakati Wasudan walipokuwa wakijaribu kufufua serikali ya kidemokrasia ya utawala wa kiraia baada ya miongo kadhaa ya utawala wa kijeshi.

Siku ya Jumatatu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alitoa wito tena kwa pande zinazozozana "kusimamisha uhasama mara moja" akionya kwamba kuongezeka mapigano kutaivuruga nchi hiyo na eneo hilo la Afrika."

Taasisi za kikanda zikiwemo Umoja wa Afrika, kundi la kikanda la IGAD, na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League), zimesema zinazungumza na mahasimu mbalimbali hasa majenerali hao wawili, kujaribu kusitisha mapigano.

Hivi sasa kuna wasiwasi kuwa mapigano ya Sudan yatapanuka zaidi na kukumuisha makundi mengine ya wanamgambo na wabeba silaha.

Sadegh Mukhtar Ahmad, msemaji rasmi wa makundi ya wapiganaji yaliyotia saini makubaliano ya amani ya Abuja, alisema katika mahojiano na waandishi habari kwamba: Kuna wasi wasi kwamba iwapo vita kati ya jeshi na RSF vitaendelea, baadhi ya makundi yenye silaha yataingia kwenye mzozo. Amesema katika hali hii, vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan vitashadidi na mustakabali wa nchi hii utakuwa matatani.

Chanzo #Parstoday

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)