TANZANIA NA MALAWI ZAKUBALIANA KUSHIRIKIANA KATIKA KUBORESHA HUDUMA ZA MPAKANI, KIFEDHA NA USAFIRISHAJI.

MUUNGANO   MEDIA
0

 

Tanzania na Malawi zimekubaliana kushirikiana katika kuboresha huduma za mpakani, huduma za kifedha na usafirishaji ili kuwarahisishia wafanyabiashara baina ya nchi hizo kufanya biashara kwa ufanisi na kukuza biashara zao na uchumi kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe. Humprey Polepole Aprili 27, 2023 alipokuwa akihutubia Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Malawi linalofanyika Mzuzu Malawi.

Akifafanua kuhusu uboreshaji wa huduma za kifedha, Balozi Polepole amesema benki za Tanzania na Malawi zinapaswa kushirikiana na kuunganisha mifumo ili kuwawezesha wafanyabiashara kulipia bidhaa na huduma, ushuru wa forodha na tozo kwa urahisi bila kubadilisha sarafu katika nchi husika hali inayo poteza musa mwingi na gharama kubwa. 

Kwa upande wa huduma za mipakani Balozi Polepole amesema nchi hizo zimekubaliana kutekeleza makubaliano ya Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Pamoja (JPC) iliyokutana mwaka 2022 Dar es salaam kwa kukamilisha ujenzi wa vituo vya pamoja kwa mpaka wa Malawi na Kasumulo kwa mpaka wa Tanzania pamoja na kuongeza saa za kazi kutoka saa 12:00 jioni hadi saa 4:00 usiku kuanzia mwezi Julai, 2023. 

Aidha, Balozi amesisitiza umuhimu wa kutumia ushoroba wa Mtwara (Mtwara Corridor) pamoja na Bandari ya Mbamba Bay katika kusafirisha bidhaa mbalimbali kama saruji na mbolea ambayo ina uhitaji mkubwa nchini Malawi.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda ya Malawi Bi Christina Zakeyo amesema Malawi iko tayari kuimarisha uhusiano wa kibiashara na Tanzania kwa kukamilisha orodha ya pamoja ya bidhaa (STR).

Aidha ametaja mambo mengine ambayo Malawi itayashughulikia ni pamoja na Mpaka wa Kasumulu / Songwe (OSBP) unaanza kufanya kazi; Kutatua changamoto za taasisi za Viwango, Utaratibu wa benki za Tanzania na Malawi (FDH na CRDB) ili zianze kubadilisha fedha moja kwa moja. 

Nao baadhi ya wafanyabiashara wa Tanzania walioshiriki maonyesho katika Kongamano akiwemo Bw Humoud Salim, (sekta ya Mifugo) Bw. Daniel Malagashimba (sekta ya Utalii) na Bi Genovefa Barnabas (sekta ya kilimo) wamesema kongamano hilo limeleta manufaa makubwa katika kukuza biashara zao nchini Malawi.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)