Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni ametoa wito kwa wabunge wa nchi hiyo “kutafakari upya” sheria kali dhidi ya mahusiano ya watu wa jinsia moja iliyopitishwa na bunge la nchi hiyo mwezi uliopita na kulaaniwa vikali na nchi za Magharibi.
“Ninaurudisha mswaada huu bungeni ili uangaziwe upya,” Museveni aliandika katika barua yake kwa bunge.
Tofauti inapaswa kuwekwa katika muswada huo “kati ya kuwa shoga na kujihusisha na vitendo vya ushoga,” Museveni alisema katika barua yake iliyosomwa bungeni na Naibu Spika Thomas Tayebwa.
Museveni aliandika “Kilicho wazi ni kwamba jamii yetu haikubali mienendo au vitendo vya ushoga.”
Wiki iliyopita, Rais Museveni wa Uganda alikataa kutia saini muswada huo ambao unatoa adhabu ya kifo katika baadhi ya kesi, na kutaka kuwa ni vyema ufanyiwe marekebisho.
Mwezi uliopita, Bunge la Uganda lilipitisha muswada wa sheria inayoharamisha kujitambulisha kama mtu wa uhusiano wa jinsia moja au LGBTQ na kuzipa mamlaka madaraka makubwa katika kukabiliana na raia wa nchi hiyo wanaojihusiha na uovu huo.
Aidha wanasheria wa Uganda walipitisha sheria ya hukumu ya kifo kwa watakaopatikakna na hatia ya mahusiano maovu ya jinsia moja.
Wananchi waliowengi Uganda wanasema inahitajika kuwaadhibu wanaojishughulisha na harakati za kuhamasisha uhusiano wa jinsia moja, ambazo zinatishia maadili ya kitamaduni na kidini katika taifa hilo la Afrika Mashariki.
Rais Museveni ni mmoja wa viongozi ambaye amekuwa akitangaza waziwazi kupinga mahusiano ya kingono ya watu wa jinsia moja akisisitiza kuwa, huo sio utamaduni wa Muafrika kama ambavyo amekuwa akiyakosoa vikali madola ya magharibi yanayoshinikiza kutobughudhiwa watu wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Chanzo #Parstoday.