NATAMANI TAWA IWE JOKOFU LA MAFANIKIO NA SIO GOFU - DKT. ABBASI.

MUUNGANO   MEDIA
0

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hassan Abbasi amesema anatamani kuona Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) inakuwa Taasisi ya mfano kwa kuwa na mafanikio makubwa katika utendaji na utekelezaji wa majukumu yake.

Ameyasema hayo leo Aprili 06, 2023 alipokuwa akizungumza na Menejimenti ya TAWA wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya katika Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka hiyo Mkoani Morogoro.

Ili kufikia Mafanikio makubwa katika Mamlaka hiyo, Dkt. Hassan Abbasi amebainisha Siri nane ambazo zitaisaidia TAWA kufikia malengo.

Amesema TAWA Inapaswa na malengo makubwa "Olympic Targets" tofauti na malengo ya kawaida na kuyatekeleza Kwa ufanisi.

Pia ameeleza siri nyingine ni pamoja na kufanya kazi kama timu na kufuata maadili ya utumishi wa Umma katika kuhakikisha TAWA inakuwa na mafanikio makubwa katika Kila nyanja.

Aidha ameitaka Menejimenti ya TAWA kuwekeza vya kutosha katika kitengo cha Mawasiliano Kwa kuhakikisha kinapata mahitaji ya msingi kama vile vitendea kazi vya kutosha Ili kupata matokeo yanayotarajiwa.

Sanjari na hilo, amewataka watumishi wa Taasisi hiyo kumtanguliza Mungu katika utekelezaji wa majukumu yao ya Kila siku Ili kuongeza ufanisi wao katika maeneo yao ya kazi .

Dkt. Hassan Abbasi amesema falsafa ya Wizara ya Maliasili na Utalii imejikita katika kuhifadhi rasilimali zilizopo Nchini na Kutangaza Vivutio vyote vya Utalii vilivyopo Nchini hivyo ameagiza watumishi wote wa Wizara hiyo kuongeza Kasi ya utekelezaji wa falsafa hiyo.

Katika ziara hiyo Katibu Mkuu huyo aliambatana na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Dkt. Maurus Msuha.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)